187 105 749KB
Kiswahili Pages 81 Year 2020
MABADILIKO YANAYOUMIZA
NDANI YA KANISA
D.J. SENI
ii
Hakimiliki © 2020 Daniel John Seni [email protected]
Msanifu: Eternal Word and Charity Publishing (EWCP) Dar es Salaam [+255-755-643-590] Mchapaji: Truth Printing Press. Dar es Salaam [+255764425704] Haki zote zimehifadhiwa. Hakuna sehemu ya kitabu hiki inaweza kuzalishwa tena bila ruhusa ya Mfasiri isipokuwa kwa mhakiki ambaye anaweza kunukuu vifungu vifupi vifupi katika hakiki zake; Wala sehemu yoyote ya kitabu hiki hairuhusiwi kuwekwa katika umbo lingine bila kibali cha mwandishi _______________________________________ Maandiko ya Biblia yamechukuliwa kutoka kwenye Biblia ya Kiswahili Toleo la shule inayotolewa na Swahili Union Version (SUV)
kinapatikana Shekinah Mission Centre (SMC)
[email protected] S.L.P 32807 Dar es Salaam +255 769 080 629 +255 787 907 347 Madale/Mivumoni, Joshua road, mkabala na Shule ya Msingi-Atlas/ at Shekinah Presbyterian Church in Tanzania, Dar es Salaam
Tabaruku Kwa wazazi wangu. Kwa Mwl. Boyeon Lee Kwa Mama S.N. Choi Mungu amewatumia kwa namna ya pekee watu hawa kwa kupokezana majukumu ya kunilea, kunifundisha, na kunipatia msaada; kila mmoja kwa wakati wake na kwa juhudi kubwa. Mungu awabariki sana.
i
Utangulizi Katika mataifa ya mengine siku hizi huwezi kuwa mchungaji wa kanisa linalojitambua ukiwa huna angalau Elimu ya Sekondari na kumaliza seminari. Katika nchi zingine, uchungaji imeorodheshwa kuwa mojawapo ya kazi zinazotambuliwa ndani ya serikali. Ni mojawapo ya kazi ambayo mtu lazima awe na maarifa ya Mungu na ya kidunia. Kinyume chake, katika mataifa mengine, mtu akiweza kunena kwa lugha tu, anakabidhiwa kundi. Ndiyo! Naamini katika uongozi wa Roho Mtakatifu katika kuongoza kanisa; wenye elimu na wasio na elimu ni sawa tu. Na wakati mwingine wasio na elimu yoyote wanaweza kuongoza kanisa vizuri kuliko wenye elimu. Hata hivyo, itakuwa ni kazi kubwa sana yenye kuchosha, kwa sababu mambo mengi unaweza kuyafanya kama uko gizani. Kwa kuzingatia uhitaji wa elimu ya uongozi ndani ya kanisa; uwe na elimu, ama usiwe na elimu, kitabu hiki kinakufaa kwa sababu nimekiandika katika mazingira ya uzoefu na mazoezi; kitamsaidia kiongozi yeyote ndani ya kanisa kuwa mwajibikaji ikiwa ataamua kukitumia vizuri, na kufuata maelekezo yake. Katika kitabu hiki, nimejaribu kujadili kwa kina mambo muhimu ambayo mtumishi wa Mungu akiyafanya ndani ya kanisa kuna uwezekano mkubwa wa kubadilisha kundi lake. Nimezungumzia mabadiliko ya kulifanya kanisa liwe ni kanisa hai mbele za Mungu likiwa linatimiza Utume Mkuu. Ni kweli kwamba Mungu ndiye huleta mabadiliko ndani ya kanisa, lakini ukweli huu hauondoi jukumu la kiongozi wa kanisa; mchnungaji, mzee, mwinjilisti, shemasi, mkuu wa idara, pamoja na kila muumini ndani ya kanisa. Pamoja na juhudi kubwa za viongozi wa kanisa, kuna uhitaji wa kanisa zima kushiriki katika shughuli za maendeleo ya kanisa, ili kanisa likue kwa pamoja. Mch. Daniel John Seni Shekinah Presbyterian Church in Tanzania, Dar es Salaam Desemba, 2020
ii
YALIYOMO Tabaruku ...................................................................... i Utangulizi .................................................................... ii YALIYOMO .................................................................. iii SURA YA KWANZA ....................................................... 1 TAMBUA DHANA YA KUPINDUA ULIMWENGU ................. 1
SURA YA PILI ............................................................... 8 TAMBUA AINA YA WASHIRIKA ULIO NAO ......................... 8 1.
Washirika Wanaokataa Uhalisia wa Kanisa lao ........ 9
2.
Washirika waliojikinai............................................ 11
3.
Washirika walalamikaji .......................................... 12
4.
Washirika wakosoaji .............................................. 14
5.
Washirika Walioridhika na Hali ya Kanisa ............. 15
6.
Washirika Tegemezi ............................................... 17
SURA YA TATU .......................................................... 19 TAMBUA MAMBO YA MSINGI KUANZA NAYO ................. 19 1.
Maombi Yasiyokoma .............................................. 19
2.
Fikiria mambo makubwa kuliko uwezo wako ......... 21
3.
Kubali Ukweli na Ukabili Ukweli ............................ 25
4.
Jifunze kwa Wengine. ............................................ 31
5.
Kubali Kulipa Gharama ......................................... 32
6.
Pambana na Tabia Zinarudisha Maendeleo ........... 37
7.
Kuwa Sauti ya Matumaini na Maono ..................... 42
8.
Tarajia Upinzani Kwenye Mabadiliko ..................... 48
iii
9.
Shughulika na Mahitaji ya Watu ........................... 53
10.
Kuthamini Watu Wanaokuunga Mkono ................. 58
11.
Kubali bila Majuto wengine Waondoke................... 59
12.
Zingatia Uwezo wa Washirika ................................ 61
13.
Mfanye Kila Mshirika Awe Shahidi .......................................... 62
Historia ya Mwandishi ...............................................................72
iv
SURA YA KWANZA TAMBUA DHANA YA KUPINDUA ULIMWENGU Tuanze kwa kusoma Matendo ya Mitume 17:6 “na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako.” Na pia Matendo ya Mitume 5:28 “akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.” Katika mistari tuliyosoma, tunaona maneno yanayoshahibiana; kwamba watu ambao wanazungumziwa katika Maandiko haya walifanya mabadiliko makubwa. Katika ule mstari wa kwanza, tunaona maneno haya "watu hawa waliopindua ulimwengu wamefika huko nako." Ni kauli ambayo inaonyesha kwamba, wanafunzi wa Yesu Kristo, walikuwa wamefanya mabadiliko makubwa, mabadiliko ambayo ni ya kupindua ulimwengu. Mabadiliko ya namna hii hayakuwa mepesi hata kidogo. Tunajua wazi kwamba Bwana wetu Yesu Kristo alipokuwa karibu na kuondoka, aliwaagiza wanafunzi wake akawaambia, ya kwamba Roho Mtakatifu atakapokuja kuwatia nguvu. Anasema katika matendo ya mitume 1:8 kwamba, "nanyi mtapokea nguvu akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu." Ahadi ya Bwana wetu Yesu 1
Kristo ilitimia katika matendo ya mitume sura ya pili. Kuanzia hapo tunaona wanafunzi wanafanya kazi kubwa. Makundi ya aina mbili yalikuwepo: kundi la kwanza kundi la mitume, na kundi la pili, kundi la wanafunzi wa Yesu kwa ujumla; hawa wote walifanya kazi kwa bidii. Kazi yao ilikuwa inaeleweka, na ndiyo maana katika matendo ya mitume sura ya 5:28 tunaambiwa kwamba walikuwa wameijaza Yerusalemu kwa mafundisho yao. Mafundisho ya aina gani hayo? Ni mafundisho ya ufufuo wa Yesu Kristo. Wakaanza kuwa tishio kwa watawala wa wakati huo. Tunaona wakuu wa baraza la Kiyahudi la Sanhedrini linaanza kukutana kujadili hoja mafundisho ya wanafunzi wa Yesu. Wakawaita Petro na Yohana na kuwaambia waache mara moja kuhubiri kwa jina la Yesu kwa sababu wanaleta doa kwa taifa la Israeli kwa kuonesha kwamba watu hawa walimuua Yesu. Petro na Yohana wanasema hatuwezi kunyamaza kwa sababu “hakuna jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.” Ni jina la Yesu peke yake. Jina lenye kubadilisha. Jina lenye kuokoa. Jina linaloponya. Ni Yesu peke yake ambaye alikuwa amevamia ulimwengu kwa ajili ya kuleta mabadiliko mioyoni mwa watu. Ama kwa hakika shughuli ilikuwa pevu. Roho Mtakatifu aliyekumo ndani ya mitume, hakuwaruhusu kunyamaza. Tukisoma habari za Mtume Paulo katika utumishi wake tunaweza kujifunza mambo mengi. Kupindua ulimwengu halikuwa jambo jepesi kama ambavyo leo tunaweza kudhania. Kuwaendea watu wasio na ufahamu wowote kuhusu Kristo haikuwa kwa nguvu zao wenyewe bali Roho Mtakatifu aliwatumia watumishi hawa. Kama tunavyojua, mtume Paulo kabla ya kuokoka alikuwa mtu aliyejitolea kukomesha Ukristo kama ibada ya uwongo hadi, alipokutana na Yesu Kristo. Baada ya siku hiyo, aliamua kujitolea 2
kwa nguvu zake zote kutangaza Injili ya neema ambayo ilibadilisha maisha yake. Paulo anasema kwamba alikuwa amehesabu kama hasara kila kitu maishani mwake ambacho hapo awali kilikuwa faida kwake kwa kutazama thamani kubwa ya kumjua Kristo Yesu Bwana wake (Fil 3: 8). Kwa sababu ya kujua thamani hiyo, mtume Paulo alitaka watu wengine pia wajue thamani ya Kristo kwa; kumwamini na baada ya kumwamini wawafanye na watu wengine waamini. Kama matokeo ya kumjua Yesu Kristo kibinafsi, Paulo alisema kwamba alifanya kila kitu kwa ajili ya Injili (1 Kor. 9:23). Alipigwa huko Filipi, na badala ya kupumzika, alisafiri kilometa 160 kwenda Thesalonike, akaingia katika sinagogi, akaanza kufundisha kuwa Yesu ndiye Kristo. Alipolazimishwa kuondoka Thesalonike, alihamia Beroya na kufanya vivyo hivyo! Mtu huyo hakuwa akizuilika katika kujitolea kwake kuhubiri injili ya Kristo! Alikuwa anaongoza mabadiliko ya kupindua ulimwengu mzima. Alikuwa na ndoto ya kufikia ulimwengu mzima. Nguvu iliyombadilisha. Nguvu ya Roho Mtakatatifu ilikuwa inamsukuma Paulo kubadilisha ulimwengu mzima. Kupindua ulimwengu. Watu wa namna hii ni wachache sana; lakini miongoni mwa wachache ni wewe! Wewe unayeishi katika ulimwengu wa sasa unaweza kufanya mabadiliko makubwa kuliko aliyofanya Paulo ikiwa tu utakubali Bwana akutumie katika kazi yake. Bwana Yesu anatafuta watu ambao watapindua ulimwengu wao. Tunaposema kupindua ulimwengu hatumaanishi kwamba tunataka kuteka serikali zilizopo madarakani, kazi yetu ni moja tu; kuhakikisha kwamba tunawafikia watu wengine kwa ajili ya Injili. Si kuwafikia tu
3
kimaono, bali tunawafikia katika hali halisi na kuwafundisha neno la Mungu. Mungu anatafuta watu ambao wanaweza kuongoza mabadiliko katika makanisa au katika kuhubiri walisafiri katika ulimwengu wa wapagani kabisa ili kumtangaza Kristo. Na ndipo tunasikilia kilio cha watu wa Thesalonike, “Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako.” Ni kilio katika mji. Watu wanaopindua ulimwengu. Watu wangapi? Watu wanne tu? Kwa sasa tunawaona ni watu wanne, lakini ukweli ni kwamba hawa watu walikuwa wamefundisha watu wengine kufanya vilevile na matokeo yake kilio kinafika Thesalonike. John Wesley aliwahi kusema, "Nipe wanaume hamsini ambao hawapendi kitu chochote ila Mungu na hawaogopi chochote isipokuwa dhambi, nami nitaubadilisha ulimwengu!" Huyu alikuwa na ndoto ya kubadilisha ulimwengu mzima. Kila mtu ndani ya kanisa amepewa uwezo wa kuwafikia watu wengine. Kila mtu ndani ya kanisa anayo nafasi ya kufanya mabadiliko katika kanisa lake. Katika kitabu hiki nitazungumzia kubadilisha kanisa la Mtaa. Makanisa mengi ya mtaa hayatimizi wajibu wake ipasavyo. Wajibu wa kanisa nini? Mojawapo ya wajibu wa kanisa ni kuwafikia watu walio nje kwa ajili ya kuwahubiri. Kuwafikia watu wasiookoka. Kuna watu ndani ya kanisa ambao hawana Habari na masuala ya kuhubiri Injili; wanaona ni jukumu la mchungaji, ni jukumu la mwinjilist, ni jukumu la mzee wa kanisa, ni jukumu la shemasi, ni jukumu la fulani; yaani wao wanajiondoa! Kwa kuwa washirika wetu wanajua ndivyo ilivyo, basi ni vigumu sana kuwepo kwa mabadiliko katika makanisa yetu ya mitaa.
4
Makanisa mengi ya mitaa hayana programu yoyote ya kuwafikia watu walio nje. Hayana bajeti yoyote kwa ajili ya kazi ya kuinjilisha. Wana bajeti ya kuita kwaya kubwa kanisani ili iimbe kwa nguvu; wala sikatai mawazo haya, lakini ninachosema ni lazima kuwepo na programu maalumu ya kupindua mtaa wenu. Unaweza kushangaa hata majirani hawajui kwamba kuna kanisa jirani yao. Kanisa limepoa kabisa, linaelekea kufa. Mchungaji amekuwa ni mtu wa kawaida kabisa, hana tofauti yoyote na watu wengine! Washirika hawana Habari na kuwaleta watu wengine kwa sababu wamejikinai wenyewe. Wamebaki na historia tu kwamba wao ndio waanzilishi wa kanisa, lakini ukiwauliza kwamba umeleta wangapi ndani ya kanisa watakujibu, “watu wanakuja wenyewe tu kwenye kanisa letu.” Nini Maana ya Mabadiliko Sasa? Ukisikia neno “mabadiliko” unapata picha gani katika ufahamu wako? Kwa tafsiri ya ujumla mabadiliko ni hali ya utofauti kutoka hatua moja kwenda hatua nyingine. Mabadiliko yanaweza kuwa hasi au chanya; yote hayo ni mabadiliko. Mabadiliko yako kwenye nyanja mbalimbali. Mabadiliko yanapotokea sehemu yoyote ile, mara nyingi yanakabiliwa na changamoto kubwa kwa sababu ya uelewa wa watu. Katika kitabu hiki, ninazungumzia mabadiliko chanya ndani ya kanisa. Ninalenga hasa kuzungumza na viongozi wa kanisa; kama vile wachungaji, wazee, mashemasi, wainjilisti, na viongozi mbalimbali wa idara ndani ya kanisa. Ninatamani kila kiongozi katika eneo lake awe kiongozi wa mabadiliko. Wewe ukiwa kama kiongozi wa idara ndani ya kanisa haupo hapo kwa ajili ya kuwafurahisha watu unaowaongoza, bali upo kwa ajili ya kuwaongoza watu kufikia mabadiliko ya kweli. 5
Kwa kawaida mabadiliko hayana mwisho. Binadamu kwa asili ni mtu wa mabadiliko. Hawezi kukaa katika eneo moja kwa muda mrefu, hivyo basi kiongozi ambaye anafurahia wakati wake pasipo kuongoza mabadiliko chanya ni kiongozi asiyefaa. Umekuta idara au kanisa liko katika hali fulani, tamani lifike katika hatua fulani. Mabadiliko yanayoumiza ni mabadiliko ambayo kwa namna yoyote ile lazima yatokee. Yaani haya ndiyo mabadiliko ambayo waswahili wanasema “punda afe mzigo ufike.” Ni mabadiliko yanayoumiza kwa sababu yataumiza watu wengi, yataacha watu wengi lakini yatavuna watu wengi kwa Bwana. Ni mabadiliko yanayoumiza kwa sababu yanaweza kukuumiza wewe unayeongoza mabadiliko hayo, pamoja na wale unaowaongoza. Watu wengine wanaweza kuhama kanisa lako kwa sababu ya mabadiliko unayoyaongoza. Na ndiyo maana nasema ni mabadiliko yanayoumiza. Ni mabadiliko yanayoumiza kwa sababu yanahitaji gharama kubwa sana. Unahitaji pengine gharama za maombi, fedha, NA muda. Mabadiliko yanayoumiza yanadumu muda mrefu, mabadiliko ambayo hayaumizi hayadumu muda mrefu. Kazi inayodumu muda mrefu, inaumiza. Kitabu hiki kinalenga kuelezea namna ambavyo kiongozi wa kanisa anavyoweza kuongoza mabadiliko au uamsho ndani ya kanisa au idara ya kanisa anayoingoza. Kwa kawaida, mtumishi unapokuwa unaanza huduma unatamani kanisa lifike mahala fulani. Kama ni kanisa ambalo tayari lilikuwa limeanzishwa na mtu mwingine, unatamani mabadiliko yatokee ndani ya kanisa kwa haraka iwezekanavyo. Mabadiliko ya wazi ambayo huwa tunapenda kuyaona ni kuongezeka kwa watu ndani ya kanisa, washirika 6
kujishughulisha na kazi ya Mungu (yaani watu hawasukumwi, bali wanajitoa wenyewe kwa kazi ya Mungu). Hata hivyo, mabadiliko haya hayaji kwa siku moja, kuna michakato ambayo kiongozi yeyote anayetamani mabadiliko anahitaji kujua na kufanyia mazoezi michakato hiyo. Jambo ambalo nahitaji kuliweka wazi hapa ni kwamba kiongozi wa mabadiliko, mchungaji, unahitaji kufikiri mambo makubwa yasiyo ya kawaida. Kama mtumishi wa Mungu unafikiria mambo madogo, basi haina maana yoyote kufikiria mabadiliko. Huwezi kupindua ulimwengu kwa mawazo ya chini. Mara nyingi tunapanga mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu, na kwa hiyo yanapotokea hatuoni muujiza wowote kwa sababu tunadhani kwa sababu ya nguvu zetu yamewezekana. Sasa ili usiingie kwenye majaribu ya namna hii inabidi uwaze na upange mambo makubwa. Uwaze mambo yanayokuzidi. Mtu mmoja aliwahi kusema, “tunapaswa kuwa na maono yenye ukubwa wa Mungu kwamba kama Mungu asipofanya haitatokea kamwe.” Mabadiliko, ni kupindua ulimwengu, kupindua mtaa wako, kubadilisha mambo ambayo hayako sawa kanisani kwako ili yawe sawa. Mabadiliko tunayozungumzia ni ya kuwaona washirika wote wakishiriki katika kazi ya kupindua ulimwengu kwa mafundisho ya Kikristo. Kwa namna moja ama nyingine tunapozungumzia mabadiliko tutakuwa tunamaanisha maendeleo. Kutoka hatua moja kwenda nyingine. Katika sura zifuatazo nitajikita katika kueleza mambo ya msingi kujua na kutenda kwa mtumishi wa Mungu yeyote ambaye anataka kufanya mabadiliko au sehemu ya mabadiliko ndani ya kanisa.
7
SURA YA PILI TAMBUA AINA YA WASHIRIKA ULIO NAO Kabla hujaanza mabadiliko yoyote ndani ya kanisa au kwenye kikundi unachokiongoza, ni lazima ujue unao watu wa aina gani. Kujua watu kunasaidia kupambana na changamoto ambazo utakabiliana nazo katika mabadiliko unayoyaongoza. Ni heri uwe mtu wa mabadiliko kwa sababu bila mabadiliko kanisa linaweza kuyumba. Ingawa siyo rahisi kuelezea kila aina ya waumini ndani ya kanisa, lakini kumbuka kwamba kanisani kwako kutakuwa na watu wenye elimu na wasio na elimu, maskini na matajiri, vijana na wazee, wenye ndoa na wasio na ndoa, na wengineo wengi. Kiongozi kanisani ni kama daktari: kabla ya kutoa dawa kwa mgonjwa, ni lazima kwanza ajue mgonjwa anaumwa nini, mgonjwa anahitaji nini. Katika Maisha ya kanisa kwa ujumla kuna sifa moja tu inayotuunganisha kwamba “wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23). Hapo ndipo tunafanana, lakini maeneo mengine yote wanadamu wako tofauti, na hivyo lazima ujue utofauti huo ili uweze kuongoza mabadiliko. Unahitaji kuwajua waumini kwa sababu si kila mmoja atapokea mabadiliko. Kuna watu ndani ya kanisa ukitaka kufanya mabadiliko yoyote wanakupa historia ya kanisa hilo kuanzia mwanzo mpaka mwisho. Watakueleza ni kwa jinsi gani lilianzishwa, 8
na ni nani alitoa kiwanja cha kanisa, na kuna wachungaji au wazee wa kanisa au mashemasi wangapi waliwahi kutumika. Watakupachika majina mengi ya utani ambayo mwenyewe huwezi kuyapenda. Na kwa sababu hiyo, ni lazima ujue waumini ndani ya kanisa. Mchungaji Rainer, katika kitabu chake cha “Who Moved My Pulpit?” (nani amehamisha minbari yangu) anasema kwamba linapokuja suala la mabadiliko, kuna watu wa aina tano ya washirika ndani ya kanisa ambao lazima uwajue kabla hujaanza kufanya mabadiliko yoyote ili wasikusumbue wakati utakapoanza.
1. Washirika Wanaokataa Uhalisia wa Kanisa lao Watu hawa ni wale ambao wamekuwepo ndani ya kanisa kwa muda mrefu kiasi kwamba mioyo yao ilishakuwa ganzi na kwamba hawaoni tatizo lolote ndani ya kanisa. Yaani kwao wanaona mambo yote yako sawasawa tu. Hawa hawajali kama ibada fulani wamekuja watu wachache, au wamekuja watu wengi. Kwao wanaona ni sawa tu. Ufuatao ni ushuhuda wa Rainer alipokuwa ameenda kwenye kanisa la miaka mingi kuwa mchungaji. Kwa tafsiri isiyo rasmi anasema kwamba kabla hajafanya mabadiliko yoyote ilibidi kwanza afanye utafiti kwa nini kanisa lilikuwa linashuka mahudhurio kila siku. Anasema kwamba: “Kazi yangu ya msingi ilikuwa kuhoji washiriki wa muda mrefu. Ushuhuda wa kupungua waumini kanisani ulikuwa wazi na wa kutatanisha. Mahudhurio ya ibada yalikuwa chini kutoka 350 hadi 180 katika miaka mitano. Kanisa lilikuwa likielekea mautini. Katika moja ya mahojiano yangu, nilimhoji mwanamke mwenye umri wa miaka
9
sabini. Alikuwa kanisani kwa karibu nusu karne. Nilimwuliza anafikiria nini husababisha kupungua kwa watu katika kanisa hilo. Cha ajabu, ingawa nimewahi kufanya huduma ya ushauri kwa muda wa zaidi ya miongo mitatu, mwanamke huyu alinishangaza kwa majibu yake: "Kanisa letu halijapungua. Nilimwonyesha grafu ya mahudhurio. Lakini alikana usahihi wake. Nilimwuliza ikiwa aligundua viti vingi viko wazi katika ibada. Alijibu “sijui.” Nilimuuliza ikiwa anamjua mtu yeyote ambaye ameacha kuja kanisani. Hakuweza kukumbuka. Nilikata tamaa kabisa kwa majibu ya mwanamke huyu ambaye amesali miaka zaidi ya arobaini kanisani hapa”."1
Mtu anayekataa uhalisia wa hali ya kanisa ni vigumu sana kuongoza mabadiliko kwa sababu haoni tatizo. Kumbe chanzo cha kujua kwamba unahitaji mabadiliko ni kujua kwamba kuna tatizo. Ukiwa na watu wa namna hii ndani ya kanisa: ambao hawajui kila kitu kinachoendelea huwezi kuongoza mabadiliko kwa sababu washirika wenyewe wanaukataa ukweli. Waumini kama hawa hawajali kitu chochote ndani ya kanisa. Wao huja kusali tu na kuondoka. Yaani ibada inapokwisha, hawana muda wa kusalimiana hata na waumini wengine. Wao wanajua kwamba kanisa ni la mchungaji, na hakuna tatizo lolote ndani ya kanisa. Namwelewa mwanamke huyu kwa sababu pengine yeye kwenye ibada alikuwa anakaa mstari wa mbele ndani ya kanisa, na ibada ikiisha anaondoka. Watu wa namna hii unahitaji kuwajua ili uanze kutoa elimu kwao kwanza kabla hujaanza hatua yoyote ile ya mabadiliko. Na kama usipowajali, hawa ndio watakuwa changamoto kubwa kwako katika kubadilisha kanisa hilo. 1
Rainer, Thom S. Who Moved My Pulpit? (p. 18). B&H Publishing Group. Kindle Edition.
10
Kumbuka wewe ni mjumbe wa mabadiliko ndani ya kanisa lako. Mungu anataka kukutumia kuamusha watu ambao wamelala. Shughulikia watu wa namna hii kanisani kwako mapema sana. Waeleze ukweli, usifumbe fumbe ukweli. Ukweli kwamba kanisa letu haliendelei vizuri unasaidia. Waambie wazi kwamba wanahitaji kujua ukweli huo, na kwamba wewe unatamani kuona mnatoka hatua hiyo kwenda hatua nyingine.
Hebu tumia dakika 5 kufikiri juu ya washirika kanisani kwako. Je kuna washirika wa namna hii. Je utafanyaje kwa ajili ya kuwasaidia kupokea ukweli wa kanisa?
2. Washirika waliojikinai Hawa ni washirika ambao hawataki kuona kitu chochote kipya ndani ya kanisa kwa sababu wamejikinai na hali iliyopo ndani ya kanisa. Hawa wanaona kanisa ni kama kilabu ya kukutana na marafiki zao tu. Ni watoaji wazuri kanisani lakini tatizo pia ni kwamba wao huona matoleo yao ya kifedha kama haki ya kupata pesa na upendeleo. Wao humfanya wachungaji na viongozi wengine wa makanisa wajione dhaifu, na pengine wanaweza hata kusema "Unajua tunalipa mshahara wako." Washirika wa namna hii hupenda hata kuamrisha namna ibada inavyopaswa kuendeshwa, na pia unaweza kushangaa kwamba hata wanapoongea na kiongozi huongea naye kwa dharau kubwa. Wanaamini kwamba wanaweza kupata kitu chochote kile wanachotaka ndani ya kanisa. Unaweza pengine hata kuwasikia wakisema kwamba yule tumemshika tumemshika sisi, hawezi kutufanya kitu chochote. 11
Ukikutana na waumini wa namna hii, wewe kama kiongozi ndani ya kanisa unahitaji kuwafahamu vizuri na uweze kuendana nao. Huwezi kuwafukuza ndani ya kanisa kwa sababu matokeo yake yanaweza kuwa mabaya kuliko unavyotarajia. Hata hivyo tutaona zaidi kule mbele kwamba unahitaji kuamua kuwakumbatia watu wa namna hii au kuachana nao.
Hebu fikiria dakika 5. Je kuna washirika wa namna hii ndani ya kanisa? Utafanyaje kama watu wa namna hii wanakukaribia kwa karibu na kujaribu kukusaidia katika mahitaji yako, lakini wanapinga ajenda zako za maendeleo ndani ya kanisa?
3. Washirika walalamikaji Hawa ni aina ya washirika ambao hawakubali makosa yao, bali hutupa lawama kwa mtu mwingine ndani ya kanisa. Yaani wao wako tayari kulaumu kuliko kutii kitu chochote: Sikiliza kauli hizi: Kanisa letu haliongezeki kwa sababu ya mchungaji wetu. Ni kosa la kiongozi fulani. Ikiwa kiongozi wetu angekuwa kiongozi bora, kanisa letu lingekuwa bora zaidi. Kwanza kiongozi wetu hata hatangazi matoleo ya kanisani, mimi hata sielewi. Jamii yetu ingekuwa imechanganyikana, yaani kanisa hili palikuwa hapatoshi, tatizo hapa ni ukabila sana. Unajua bwana, yaani kanisa letu halipendwi hapa mtaani! ni kosa la baadhi ya washirika kwa sababu ni wazinzi, watu hawataki kuja kanisani. Mwingine utakuta anasema “Ni kosa la makanisa mapya hapa mjini, kwa nini huyu amepanda kanisa hapa karibu na sisi? Mwingine "Sielewi kwanini makanisa haya mapya yanapandwa karibu na sisi. Kwanza tayari tunayo 12
kanisa karibu kila mtaa. Yaani wangebaki huko huko walikokuwa, kanisa letu lingekuwa sana. Mara utasikia wanasema kosa la wazee wa kanisa; hawa wazee hawafanyi kazi vizuri, sisi tumejitahidi kutekeleza bajeti waliyotuletea lakini hakuna maendeleo yoyote yanayotokea ndani ya kanisa. Tatizo ni mama mchungaji wa kanisa hili hana moyo wa utumishi kabisa na hawezi kuwakusanya wakina mama wa kanisa letu. Kosa ni waumini wachanga kwa sababu wanayumba yumba kwenye imani. Siku hizi mahubiri ya mchungaji ni marefu sana na pia hayana mvuto wowote, kwa hiyo watu hawaji kwenye ibada zetu. Kama kanisa likiwa na watu wengi wa namna hii, basi unahitaji mabadiliko yanayoumiza. Ukiangalia kwa makini lawama hizo zote, hakuna lawama hata moja ambayo watu hawa wameielekeza kwao, bali wananyoosha vidole kwa watu wengine tu. Hawa watu wanaamini kwamba matatizo yaliyopo ni kwa sababu ya mtu mwingine hajatimiza wajibu wake. Ni sawa. Lakini mbona wao hawatimizi wajibu? Watu wa namna hii ndani ya kanisa wapo, na wewe kama kiongozi utawasikia kwa masikio yako mwenyewe, au kwa kuletewa habari zao. Hivyo basi ni lazima ujue uwepo wa kundi hili ili uweze kuongoza mabadiliko yanayoumiza. Na unahitaji kuomba hekima ya Roho Mtakatifu namna ya kushughulika na waumini wa namna hii.
Fikiri dakika 2 na fikiri watu waliopo kanisani kwako wenye tabia kama hizi. Je kuna watu wa namna hii kanisani kwako? Tumia muda kuwaombea.
13
4. Washirika wakosoaji Wakosoaji ni kama walalamikaji kwa sababu wanaamini pia kwamba shida katika kanisa ni kosa la mtu mwingine. Lakini tofauti na walalamikaji, wakosoaji ni hatari zaidi kwa sababu wanasumbua sana viongozi wengine na kuwavunja moyo. Wakosoaji watakuambia moja kwa moja juu ya hisia zao. Watakuambia uso kwa uso au kwa namna nyingine lakini lazima wakwambie kosa lako tena bila aibu. Wakosoaji ambao ni wabaya zaidi ni wale ambao wanaitwa PAST (People Are Saying That-Watu Wanasema Hivi). Wakosoaji wa namna hii wanakuwa na matatizo makubwa kwa sababu wanatumia watu wengine kuwasilisha mawazo yao. Watakuja kanisani na kuanza kusema wazi kwamba, watu wanasema mchungaji wetu ni mzembe. Kwa namna moja au nyingine wao wanajaribu kujiondoa katika tuhuma za mchungaji, na wanaonekana kuwakilisha kundi kubwa. Kusema kweli, wakosoaji watakuambia namna mpango wako wa kuleta mabadiliko usivyowezekana. Watatoa sababu za kutosha na kukosoa waziwazi utendaji kazi wako. Wakiwepo watu wa namna hii, huna haja ya kukata tamaa, unapaswa kujua namna ya kwendana nao. Kwa kweli wakosoaji kwa namna fulani wanakuwa na mchango mkubwa wakati mwingine katika maendeleo ya kanisa. Kuna wakosoaji ambao watakuambia moja kwa moja makosa yako na udhaifu wako bila kuzingatia muktadha. Hawa wanaweza kuwa chachu kwako ya kuendelea zaidi na zaidi katika huduma. Unahitaji kuwa na moyo mkuu kwa ajili ya kupokea ukweli. Kama wakosoaji
14
hawa wanasema ukweli, basi inabidi ukubali kuukabili ukweli, siyo kuwachukia.
5. Washirika Walioridhika na Hali ya Kanisa Hawa ni waumini wa muda mrefu ndani ya kanisa, lakini ni wepesi wa kukwazika. Watu hawa hawapendi kuona kiongozi anaanzisha kitu kipya kwa sababu wameridhika na hali ya kanisa. Yaani wao hawaoni kitu chochote kile kinachohitaji kuboreshwa. Wamezoea kukaa kwenye viti vilevile, wamezoea kuona rangi ya kanisa hiyohiyo, wamezoea kuona mapambo ndani ya kanisa hayohayo. Kwa mfano washirika wa namna hii niliwahi kuwaona katika kanisa moja hapa nchini. Wao wanashikilia mapokeo ya kanisa kwa hali ya juu sana na wameyafanya kuwa sehemu ya Biblia. Nikiwa chuo kimoja cha Biblia nilikutana na waumini wa namna hii; ambao walikuwa ni wanafunzi wenzangu. Kanisa letu lilikuwa haliruhusu watu kuomba kwa pamoja. Alikuwa anachaguliwa mtu mmoja tu kuwasilisha maombi na wengine mnaitikia “ameni.” Sasa siku moja mimi na rafiki yangu mmoja tuliamua kufanya maombi kwa njia nyingine. Tulitaka kuanzisha uamsho ndani katika chuo hicho. Maombi ya usiku yalipoanza: mimi nilikuwa kiongozi wa ibada, na rafiki yangu alikuwa ni mhubiri. Alipomaliza kuhubiri niliwaambia watu kwamba “leo tunaenda kuomba kwa pamoja.” Watu wakawa wamenyamaza tu. Lakini nyuso za wengine zilionekana kuwa na furaha. Nikagundua kwamba kuna watu hawataki kuomba kwa pamoja, na kuna watu wanataka tuombe kwa pamoja. Sasa mimi nikaona kwamba wanaotaka tuombe kwa pamoja ni wengi. Basi nikaongoza wimbo wa kuabudu (wao 15
wanauita wimbo wa kuvuta). Tulipoanza kuabudu, nguvu za Roho Mtakatifu zilijaa kwenye darasa hilo. Mara tukaanza kuomba kwa pamoja! Hata dakika moja haikuisha; binti mmoja aliangushwa na mapepo. Basi wengine wakaendelea kuomba, huku wengine wanakemea pepo. Na yule binti alifunguliwa usiku ule. Unaweza ukaona namna ilivyokuwa, kwamba tulikuwa tunafanya ibada kila siku, na hakuna siku ambayo pepo alilipuka, lakini siku ile kwa sababu tulikusudia kuwasha moto, basi pepo aliona hiyo sehemu haimfai. Unajua kilichoendelea? Kesho yake kundi fulani la wanafunzi walienda kwa mkuu wa chuo kushtaki kwamba sisi tumeanza kuleta mafundisho ya kigeni, tunakemea pepo ndani ya ibada, tunafanya ibada ya makelele. Walinukuu maandiko kadhaa kuhusu maombi ya kupiga kelele. Mimi na rafiki yangu tuliitwa ofisini. Tuliwaambia kwamba wanaolalamika waje, ili tuzungumze kwa pamoja, maana sisi hatuoni kosa lolote. Mkuu wa Chuo kwa hekima alituambia msifanye maombi ya namna hiyo kwenye ibada, ama sivyo subirini ibada iishe, halafu mwendelee. Tukakubali. Kilichoendelea pale ni kwamba hata tulipoendelea kuomba baada ya ibada, wanafunzi wengine walitushitaki tena kwamba tunawapigia kelele. Watu wa namna hii wapo ndani ya makanisa. Kama kiongozi lazima uwafahamu vizuri kabisa. Wanakwazika hata ukikosea kukiri “imani ya mitume.” Tena wanaifanya kuwa kesi kubwa na unaweza ukashangaa kesi hiyo ikafika mpaka kwa viongozi wa ngazi ya juu ya kanisa. Kwa kosa la kukosea kukiri imani ya mitume. Kosa ambalo pengine wangevumilia tu, lisingejirudia. Kosa la kuhubiri unatembea minbarini linaweza kusababisha kufukuzwa mchungaji kwa sababu ameenda kinyume na mazoea ya kanisa. 16
Kwa namna moja ni watu wanaoshika tamaduni zaidi kuliko hata neno la Mungu. Kwa mfano unakuta wanafuatilia mambo ya mavazi ndani ya kanisa. Kwao injili ya mavazi ndiyo injili. Kumbe injili ya mavazi siyo injili bali ni mahubiri ya maadili tu. Utawasikia wakisema “kuvaa suluari kwa mwanamke ni dhambi kubwa” maana imeandikwa “mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanamume.” Utakuta wanakemea uvaaji wa sketi fupi, huku wakiacha mambo ya msingi yaliyo kwenye neno la Mungu. Mimi sisemi kwamba masuala ya mavazi yasizingatiwe ndani ya kanisa, lakini ninachojaribu kusema ni kwamba kuna zaidi ya hapo. Vilevile unaweza kukuta wanakwazika tu kwa kuona wanakwaya wanacheza wakati wa kuimba. Utakuta wanasema “kanisa limeharibika.” “Mchungaji huyu anaharibu kanisa letu.” “Wanakwaya siku hizi wamekuwa ni wahuni tu.” “Wanaimba nyimbo za ajabu ajabu.” Unakuta mtu kama huyu anakwazika na pengine kufikia hatua ya kuhama kanisa. Kanisa likiwa na watu wa namna hii wengi, haliwezi kubadilika, mpaka mchungaji au kiongozi atakapoamua kufanya mabadiliko yenye kuumiza.
Ni tukio gani ambalo ulilifanya kanisani kwako likaonekana limeenda kinyume na mazoea ya washirika? Ni kwa namna gani ulilishughulikia? 6. Washirika Tegemezi Washirika hawa wanaona kwamba kiongozi ni lazima atatue matatizo yao. Yaani waumini wa namna hii wanapenda kufanyiwa mambo kiupendeleo zaidi. Wao hujiona wana haki kuliko wengine. 17
Washirika wa namna hii wanafikira kwamba mchungaji ni lazima atatue matatizo yao yote. Kuna kitu kimoja hawa watu hawataki kukijua kwamba mchungaji au kiongozi naye ana matatizo kama wao. Yeye amechaguliwa kuwa kiongozi tu, lakini haimaanishi kwamba kuwa kiongozi anakuwa hana matatizo. Tofauti ya kiongozi na wengine ni namna ambavyo anashughulikia changamoto zake. Washirika wa aina hii wanamtegemea kiongozi wao kwa kila jambo. Wanamtegemea awatembelee majumbani kwao (jambo ambalo ni zuri) lakini wao hawako tayari kuwatembelea waumini wenzao kwa sababu wanaona hiyo siyo kazi yao. Nakumbuka nikiwa mwinjilist kwa mara ya kwanza nilikuwa naongoza kanisa ambalo waumini karibu asilimia 95 walikuwa ni wanawake. Sasa kila Jumapili nikiwa na matangazo na kuwataka kujadili walikuwa wananiambia kwamba, “jadili tu mwenyewe, sisi tunakuamini, chochote utakachosema tutafuata.” Kwa kweli inaonekana ni kauli nzuri, lakini bado ni kauli ya utegemezi. Hawa washirika hawakuwa na mawazo mbadala kwa sababu walinitegemea mimi. Wao hawawezi kuuliza kwa nini, wao wanasema tutafuata tu. Ni utii wa aina yake, hata hivyo utii kama huu unahitaji kiongozi shupavu ambaye atawaongoza watu hawa kuelekea mabadiliko.
Je kanisani kwako kuna “washirika tegemezi” linapokuja suala la maendeleo ya kanisa? Utawasaidiaje?
18
SURA YA TATU TAMBUA MAMBO YA MSINGI KUANZA NAYO Katika kuongoza mabadiliko, kuna mambo ya msingi ambayo unahitaji kuanza nayo. Katika sura ya pili tulijadili aina ya washirika ambao unapaswa kuwafahamu ndani ya kanisa. Katika sura hii nitazungumzia mambo ya msingi kuanza nayo unapotaka kuongoza mabadiliko ndani ya kanisa. Mambo haya nimeyapanga kimkakati, kwa maana ya kwamba jambo la kwanza linajenga hoja ya pili na vivyo hivyo mpaka mwisho.
1. Maombi Yasiyokoma Maombi ni hatua ya kwanza kabisa katika kuleta mabadiliko katika uongozi wako. Huwezi kuleta mabadiliko ya kweli kama huombi. Viongozi wakubwa wa kiroho duniani katika historia walioleta mabadiliko walikuwa ni watu wa maombi sana. Walikuwa wanafunga na kuomba kwa ajili ya kuhitaji msaada wa Mungu katika maisha yao. Tunayo mifano katika Biblia. Hebu tuangalie Nehemia alivyoleta mabadiliko makubwa. Nehemia anasikia habari kwamba ukuta wa Yerusalemu umevunjika vipande vipande. Nehemia alihuzunika kusikia habari hizi zenye kutisha za juu nchi yake. Unakumbuka alichofanya? Aliomba na kupata ruhusa kutoka kwa Mfalme Artashasta ili kurudi Yerusalemu, na mara moja akaanza kuongoza watu kujenga ukuta. Hata hivyo kabla ya kufikia katika hatua hii Nehemia alifanya jambo muhimu sana. Nehemia 1: 4: 19
“Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni.” Neno linasema kwamba Nehemia akafunga na kuomba kwa siku kadhaa kabla ya kuchukua hatua za kuleta mabadiliko. Alijua hangeweza kuongoza juhudi hii bila hekima, nguvu, na ujasiri kutoka kwa Mungu. Nehemia hakutaka kutegemea mbinu zake binafsi au ujanja wake katika kuleta mabadiliko hayo, bali aliomba kwa bidii sana. Bila maombi hatuwezi kuleta mabadiliko yoyote katika huduma tulizo nazo. Yawezekana kanisa lako limekuwa katika changamoto za ukuaji kwa muda mrefu. Yawezekana unajua wazi kwamba unahitaji kufanya mabadilio fulani lakini unaogopa, au pengine hujui ni mabadiliko ya aina gani yanahitajika. Suala hapa siyo kubadilisha uongozi wa kanisa. Unahitaji kuomba hekima ya Mungu. Au umejaribu kufanya mabadilio kidogo na watu wamekushambulia? Unahitaji kuomba. Unahitaji kuomba ujasiri kutoka kwa Mungu ili kila hatua unayoipitia uwe na uhakika kwamba imepata kibali mbele za Mungu. Kuongoza mabadiliko kanisani maana yake ni kuonyesha msitakabari wa kanisa lako. Kanisa ambalo halina msitakabari ulio wazi haliwezi kubadilika. Na hatuwezi kufikia msitakabari wetu bila kuwa watu wa maombi. Haitoshi tu kusema kwamba tunamsubiri Yesu. Ndiyo, tunamsubiri Yesu. Lakini wakati tunamsubiri Yesu tunafanya nini? Bila maombi, wazo lako zuri litakuwa wazo baya. Siku zote Shetani anaangalia jambo zuri na analibadilisha linakuwa baya. unaweza kushinda kwa njia ya maombi. Shirikisha kanisa zima kwa ajili ya maombi ya jambo ambalo mnataka kulibadilisha. Mara 20
nyingi katika huduma zetu tunahangaika na mahudhurio machache ndani ya kanisa. Sasa ili kuweza kushindana na changamoto hii, lazima tuombe.
2. Fikiria mambo makubwa kuliko uwezo wako Kwa kawaida watumishi hupenda kunukuu Warumi 12:3 inayosema, “maana kwa neema niliyopewa nawaambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha Imani yake.” Hata hivyo, maana ya Kiswahili ya fungu hili kwa kweli inaweza kumpoteza mtu akashindwa kuwa na maono makubwa kwa kuogopa kunia makuu. Hapo haimaanishi kutokufikiria maono makubwa, bali ni “kujifikiria mwenyewe binafsi.” Biblia inakaza kujifikiria mwenyewe kuliko wenzako. Kwa hiyo kufikiri juu ya maono makubwa ni muhimu sana. Je kiongozi unawaza kuwa na kanisa la aina gani? Unawaza kuwa na washirika wangapi? Ninaona jambo hili liwe la msingi baada ya kumwomba Mungu kuhusu mabadiliko au hata huduma ambayo unawaza kuwa nayo. Kama mawazo yako kuhusu huduma yako ndani ya uwezo wako, basi pengine huhitaji mabadiliko yoyote au kwa lugha nyingine maendeleo yoyote kwa sababu tayari umekwisha kuridhika. Hata hivyo, kuna faida nyingi kwa mtumishi wa Mungu kuwaza mambo makubwa kuliko yaliyo ndani ya uwezo wake; 1. Huchochea Kumtegemea Mungu Asilimia 100 Kama ukiwa unawaza kufanya mambo madogo tu ambayo unaona kabisa katika hali ya kawaida inawezekana, basi ujue kwamba huwezi kumtegemea Mungu bali utategemea akili zako 21
mwenyewe. Na Biblia imeonya kuhusu kutegemea akili zako mwenyewe. Mith. 3:5 “Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe.” Kwa mfano ikiwa kiongozi unafikiria kuwa na waumini zaidi ya mia tano. Huku ukijua wazi kwamba pia si rahisi kwa eneo ulilopo kuwepo kwa watu mia tano; wacha maono haya yaendelee kuishi ndani yako. Kuna wakati Mungu atayatimiza. Unajua ndoto hii inaweza kutimiaje? Unaweza kupata maarifa na hekima za Kimungu kuanzisha makanisa madogo madogo ya nyumbani, sehemu tofauti tofauti. Ukawa unafanya maombi na maombezi. Kwa kweli, ingawa watu hawa hawawezi kuhudhuria kanisani, hawa watu ni sehemu ya kanisa lako. Unapokuwa na ndoto kubwa, inakusaidia wewe kumtegemea Mungu kwa sababu katika akili za kawaida haiwezekani kutimia, bali ni Mungu tu. Inabidi uwe na ndoto ambayo kila mtu akisikia anasema, “Ni Mung utu.” Kama jambo likiwa ndani ya uwezo wako, ni rahisi sana kuacha kumtegemea Mungu na kuanza kuzitegemea akili zako mwenyewe. Weka maono yako makubwa wazi. Weka kusudio lako la kuwaleta wengine kwa mwaka wazi. Usiweke maono madogo. Kwa mfano panga kwamba kila muumini alete watu 10 kwa mwaka ambao watakaa. Shikilia maono haya kwa nguvu zote. Kwa vyovyote vile lazima utamtegemea Mung utu katika kutekeleza ndoto hiyo. Nimetumia maneno “ndoto na maono” kwa maana moja. Kumtegemea Mungu kwako kuko wapi kama unajua kwamba utapata kila kitu kupitia mshahara wako? Waza mambo yanayozidi mshahara wako. Kama unawaza ndani ya mshahara wako, bado unawaza ndani ya boksi. Toka nje ya boksi. Mshahara wako hauwezi 22
kujenga kanisa. Lazima kuwepo na nguvu ya ziada. Lazima kuwepo na mipenyo mingine ambayo wewe huijui. Hapo ndipo tunasema kumtegemea Mungu. Nimekuwa na ndoto kubwa ya kujenga kanisa kubwa na la kisasa. Kwa kweli kuna mtu ambaye aliniambia kwamba atanisaidia kujenga kanisa hilo. Lakini nilipopiga hesabu ya kanisa kukamilisha kanisa hilo, nimeona hata aibu kumwambia mtu huyo. Kwa haraka haraka linagharimu dola za Kimarekani laki tatu. Hapa ndipo niliposikia sauti ndani ya moyo wangu kwamba, waza zaidi ya hapo. Nikitafakari washirika kanisani, hiyo pesa ni kubwa sana; lakini bado ninaamini kwamba dunia na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana. Na kwa sababu hiyo, nimewaza zaidi ya uwezo wangu. Waza zaidi ya uwezo wako. Hata kama uko jangwani. Waza kisichowezekana. Yasiyowezekana kwa wanadamu yawezekana kwa Mungu. (Lk 18:27) 2. Huchochea Kusubiri kwa Hamu Kusubiri kwa hamu jambo lolote lile ni muhimu sana. Unapokuwa umeweka maono yako mbele za Mungu, kuna wakati unasubiri kwa hamu uone namna ambavyo Mungu anataka kukushangaza kwa maono hayo. Hamu ya kusubiri ni kwa kila mwanadamu. katika maisha yetu haya tunayo hamu ya kuona mabadiliko yakitokea katika kipindi chetu. Mimi huwa nina hamu hata ya kuona mwisho wa dunia ukitokea nikiwa hai. Mtumishi wa Mungu ukifiri zaidi ya kile ambacho kipo ndani ya uwezo wako, hakuna jipya. Hakuna hamu ya kusubiri kwa sababu umeshajua mwisho wake. Kwa hiyo ili hamu iongezeke katika kusubiri mbele za Mungu, lazima uwaze makubwa kuliko yaliyo ndani ya uwezo wako 23
3. Kichocheo cha kuomba kwa bidii. Unajua. Unapaswa kuomba sana kwa ajili ya mabadiliko au maendeleo ndani ya kanisa lako au huduma yako. Ingawa kila mtu anapaswa kuomba, wewe unapaswa kuomba zaidi. Nini kichocheo cha maombi yako? Hata hivyo kama kuna jambo ambalo linafikirisha zaidi huwa linasababisha tuongeze maombi yetu kwa Mungu. Kama kuna jambo ambalo lipo nje ya uwezo wako na wewe unatamani kuona linatimia katika maisha yako linatamanisha kumwomba Mungu zaidi na zaidi. Kwa sababu hiyo nimesema kwamba jambo linapokuwa kubwa zaidi linakuwa ni kichocheo cha maombi kwa Bwana. Hebu watumishi wa Mungu tuache kuomba vitu vidogo vidogo. Mungu anaweza kufanya mambo makubwa sana kuliko haya ambayo tunayaomba. Yaani kila siku unaomba chakula? Kweli? Kuna mambo makubwa zaidi ambayo tunaweza kumwomba Mungu. Sikatai kuomba mambo hayo madogo madogo kwa sababu ni wajibu wetu kuomba. Lakini hoja yangu hapa ni kwamba unapokuwa na jambo kubwa la kuombea inakusaidia sana. Yaani unapaswa kuwa na jambo kubwa ambalo mpaka kufa kwako utakuwa unaliombea. Unapokuwa na ndoto ya kubadilisha kanisa ili liwe la kiinjilisti si ndoto ndogo. Ni ndoto ya kupambana na ulimwengu wa giza. Ni ndoto ya kupambana na mawazo mgando miongoni mwa washirika. Na kwa sababu hiyo unahitaji kuweka malengo makubwa na uanze kuona yakitimia kupitia maombi hayo. Kweli, matokeo ya maombi yetu si sababu za maombi yetu kwa Mungu. Mungu anajua kila kitu. Anatimiza kila kitu kwa makusudi yake. Lakini ametuagiza kuomba, kuomba kuomba.
24
Kwa hiyo tunaona kwamba kiongozi au mtumishi yeyote yule lazima kwanza yeye mwenyewe abadilike. Lazima aanze kuwaza kuliko ambavyo anawaza sasa hivi. Lazima anapokuwa kwenye maombi aone dunia yote ikiwa katika kiganja cha mkono wake. Hayo ndiyo maono ya kiongozi.
3. Kubali Ukweli na Ukabili Ukweli Kukubali ukweli haimaanishi kwamba wewe ni dhaifu, bali unaonesha kwamba una nguvu. Watu wengi siku hizi hawakubali ukweli na uhalisia kwa sababu ya kufundishwa mafundisho yasiyofaa kuhusu uhalisia. Watu wengi siku hizi wanapenda kusema kwamba “usikiri udhaifu.” Kukubali ukweli siyo kukiri udhaifu kwa njia mbaya bali ni kukubali kwamba kwenye suala fulani kuna ukweli wake. Kama kuna jambo linakusumbua lazima ukiri ukweli wake na kwamba tatizo hilo lipo na unapaswa kulikabili. Mifano tuliyozungumzia hapo juu kuhusu mama aliyekataa ukweli kwamba kanisani kwao idadi ya waumini ilikuwa haipungui ni mojawapo ya ukweli ambao watu wengi huwa hatukubali. Kwa mfano kiongozi unapokuwa kanisani lazima ukubali ukweli kama waumini ndani ya kanisa wanapungua au wanaongozeka. Mara nyingi tunatamani kupata taarifa ambazo nzuri za maendeleo. Tunatamani kuona kanisa linajaa kwa wakati mmoja. Wakati mwingine tukipewa taarifa kwamba waumini wanapungua kanisani kwetu tunazikataa na kujifariji kwamba waumini bado wapo na hatuchukui tahadhari yoyote. Kiongozi yeyote wa kanisa aliye makini lazima akubali ukweli wa tatizo ili alitafutie dawa yake. Ukikataa ukweli kwamba kuna shida ndani ya kanisa unatengeneza mazingira ya tatizo hilo kudumu kwa muda mrefu kiasi kwamba itakusumbua sana kulitatua. 25
Viongozi wengi hudhania kwamba wana muda wa kutosha kufanya mabadiliko, na hivyo wanasubiri. Hupenda kusema “kesho nitafanya” au wengine wanasema umri wangu ni mdogo sana, nitakuja kufanya mambo makubwa sana katika maisha yangu. Mwingine anakuwa na maneno tu kwamba “nitajenga kanisa kubwa sana mahali hapa.” Maneno haya ambayo mengi tunayasikia kwa wahubiri wa leo kwamba “jitamkie baraka” mengi hayasaidii kama mtu akijitamkia baraka halafu hachukui hatua za kufanya kwa muda muafaka. Inawezewekana ukawa unayo nia ya kufanya mabadiliko katika kanisa lako au katika uongozi wako, fanya sasa, acha kusubiri kesho. Kuna mambo ambayo tutayaangalia huko baadaye hatua za kufanya mabadiliko. Lakini kitu ambacho nataka kuzungumzia katika hoja hii ni kwamba acha kucheza na wakati. Acha kusubiri kufanya mambo mwishoni mwishoni. Kufanya mambo mwishoni huonesha kwamba wewe haujawa tayari kukabiliana na mabadiliko ndani ya kanisa au katika jamii inayokuzunguka. Kubali ukweli na ukabili ukweli na mambo yatabadilika ndani ya kanisa. Jukumu lako kama kiongozi wa mabadiliko lazima uwaongoze waumini wako kukabiliana na hali halisi. Halafu lazima uwasiliane nao ukweli huo na uwaambie hatua zinazohitajika kuchukuliwa ili kusonga mbele tena na tena. Mwishowe, lazima jambo hili ulione kama jambo la dharura sana. Kama mahudhurio kanisani hayaridhishi, lazima uwasiliane na watu, maana wao ndio wanaokuja kanisani. a) Ukweli Kuhusu Mahudhurio Kanisani Kuna makanisa madogo yenye weatu 10 hadi 20 haya huhitaji utafiti kujua kwamba watu wamepungua. Kwa maana kama 26
wasipokuja watu wawili tu unaweza kujua. Ili kujua kwamba mabadiliko yanatokea kanisani kwa kanisa lako kukua zaidi nambari zinaweza kusaidia kwa uwajibikaji na kwa kukabili ukweli. Ikiwa kanisa lako limepungua katika mahudhurio ya ibada kutoka 250 hadi 35 katika miaka miaka 10, kuna kitu kitu hakijaenda sawa. Maana yake ni kwamba kila mwaka watu 21 wanaondoka kanisani. Hesabu sio lengo, lakini inaweza kuelekeza makanisa yetu kwenye ukweli. inaweza kuleta uwajibikaji. Nilipanda kanisa kwa muda wa miaka 10 sasa, lakini mpaka sasa waumini wa kanisa hawajafika 200. Kila mwezi waumini wapya huja na kuondoka. Nimekuwa nikijiuliza kwa nini wanaondoka? Kila mtu kwa kweli ana sababu zake. Sasa nimeamua nitafute sababu kwa nini wanaondoka. Kama nikiangalia kwenye daftari la wageni, basi kila mwaka wageni wanaohudhuria kanisani kwangu ni zaidi ya 50, na kama wangekuwa wanabaki, basi kanisa lingekuwa na watu 500 kwa miaka 10. Usijidanganye kwenye mahudhurio ya kanisani, hakikisha kwamba unajipa ukweli. Ingawa ukweli unauma, lakini bora ukubali ukweli na uweze kukusaidia kukabiliana na tatizo b) Fanya Tathmini Kujitathimini mwenyewe si rahisi. Kwa hiyo inashauriwa kwamba tafuta mtu ambaye hajawahi kuja kanisani kwako. Mwambie atathimini mambo yote kanisani: i.
Atathmini Mazingira ya Kanisani.
Kuanzia mazingira kanisa lilivyo, (je kanisa linaakisi ibada za mahali hapo), mapambo ndani ya kanisa, vyombo vya muziki (viko juu au chini), taa ndani ya kanisa, minbari, viti, vivuli vya kupumzikia, ibada za watoto kama zipo nk. 27
ii.
Atathmini Mazingira ya ibada
Kuanzia ibada inapoanza hadi inavyomalizika. Waimbaji (kwaya), kusifu na kuabudu, matoleo, mahubiri, mhubiri mwenyewe, matangazo, mwisho wa ibada na mengineyo. Je kuna jambo gani ambalo hajalifurahia iii.
Atathmini Ukarimu
Kuanzia namna alivyoingia kanisani kama alikaribishwa au hakukaribishwa, vitu ambavyo vimemvutia kuendelea au kutokuendelea kuwepo ndani ya ibada. Kwa kweli inabidi umwambie kwamba lazima awe mkweli, na kama hawezi kuwa mkweli basi ni bora asifanye kazi hiyo. Mwambie wazi adhima yako ya kufanya zoezi hilo. Fanya hiyo kazi mara 4 kwa mwezi, kwa maana ya kwamba wageni hao tofauti tofauti na kutoka sehemu za mbali na kanisa na hawajawahi kuja kanisa wafanya tathimini. Kwenye tathimini itabidi mkubali ukweli utakaojitokeza. Kupitia ripoti hiyo, utajua kwa nini watu hawarudi tena kanisani kwako. Nimeamua kutumia mbinu hii. Wakati naandika kitabu hiki, bado nasubiri matokeo yake. Lakini Mchungaji Rainer anasema kwamba njia hii imekuwa msaada kwenye makanisa mengi. Kuna mtu mmoja aliwahi kuja kanisani kwetu mara moja tu sikumuona tena. Siku moja nilikutana naye kwenye usafiri wa umma na nilimuuliza kwa nini hakuja tena kanisani kwetu. Alijibu kwamba utaratibu wa kanisani kwetu ulimshinda. Aliona kwamba hawezi kuendelea kuja. Yaani huyu alikuwa muwazi kabisa, sasa kuna wangapi ambao siyo wawazi? Ambao wananyamaza kimyakimya? 28
Utaratibu wa ibada kumbe nao unaweza kusababisha watu wakawa wanaondoka kanisani moja kwa moja. Kuna mama mmoja alienda kusali kanisa fulani. Alipofika hapo na kumaliza kujitambulisha baadaye mzee wa kanisa akasema, “naomba mgeni wetu wa leo mama Recho (siyo jina halisi) atuongoze kwa maombi ili tumtolee Mungu sadaka. Huyu mama, ukizingatia kanisani kwake hajawahi kuomba hata mara moja kwenye umati wa watu. Alifanya jambo la busara sana. Akasema “tufumbe macho tuombe!” wakiwa wamefumba macho, mama alichomoka polepole akaenda zake nyumbani. Mama mmoja alijitolea kuendelea na maombi hayo. Wanafumbua macho, hawakukuta mtu. Hakurudi tena. Unafikirije? Ni kosa la nani? Ni kosa la mzee wa kanisa kwa sababu yeye alidhani kwamba kwa kuwa mama huyu alijitambulisha vizuri, basi anaweza kuomba pia. Inawezekana mama huyu alijua kuomba vizuri tu, lakini hana mazoea ya kuomba kwenye umati wa watu. Baada ya kupokea ripoti hiyo kutoka kwa watu ambao umewaandaa; usijaribu kujibu hoja za kwenye ripoti hiyo kama mwanasiasa anajibu hoja za chama tawala au chama cha upinzani. Unajua wanasiasa mara kwa mara huwa hawakubali ukweli. Hata kama akiambiwa ukweli huwa hawezi kukubali na badala yake hutafuta majibu ya lazima. Ukifanya hivyo, huwezi kuongoza mabadiliko ya kweli. Nimesema ni mabadiliko yanayoumiza. Kwa sababu inabidi ukubali ukweli wa ripoti iliyotolewa na ufanyie kazi badala ya kuanza kujibu hoja. Washirikishe viongozi wote kanisani baada ya ripoti hiyo. Na kisha uongozi mnapaswa mshirikishe kanisa zima kwenye vikao maalumu. Utaona mabadiliko makubwa yakitokea baada ya kufanyia kazi vipengele hivyo. 29
Hivyo basi, kufanya tathimini kujua ni wapi unakwama ni jambo la maana sana, na litakusaidia kutatua changamoto hizo. Inawezekana majibu yanaweza yasifanane kwa sababu kila mtu ana vitu anavyovipenda ndani ya ibada, lakini nikwambie wazi tu kwamba kuna vingi vitakavyofanana na vikifanana lazima uvishughulikie haraka iwezekanavyo. Nini Kifuate Baada ya Tathmini Jambo la msingi kabisa ni kwamba, “fanya mabadiliko katika mambo madogo madogo. Baada ya kuona tathmini ya maeneo dhaifu, basi anza na mambo madogomadogo. Popote pale ambapo kuna mabadiliko yamefanyika, unapaswa kujua kwamba kuna mambo madogo madogo yalianza kufanyika kwanza. Kwa mfano kama ikiwa unataka kuongeza idadi kubwa watu kanisani. Shirikisha watu kile ambacho wanaweza kukifanya. Hakikisha kwamba mtu wa kawaida kabisa ndani ya kanisa, anaweza kufanya kile ambacho unataka afanyaje. Wafanya watu wapende kazi wanayofanya. Biblia inasema kwamba watu wanapaswa kufanya kazi kwa moyo, na wala si kwa kulazimishwa. Kwa sababu hiyo, ni kazi ya mchungaji au kiongozi yeyote hakikisha kwamba wanafanya kazi kwa moyo. Ukitaka kujua Kwamba watu wanafanya kazi kwa moyo angalia namna wanavyojitoa. Angalia namna wanaoshiriki kazi za kanisa. Pia, hakikisha kwamba kila mtu anakuwa sehemu ya mabadiliko. Kama tulivyojadili hapo juu kwamba, kuna wanaweza kupinga mabadiliko, lakini hii haimaanishi kwamba watu wengine pia watapinga, kwa hivyo wale ambao wanakubaliana na wewe, basi hakikisha wanakuwa sehemu ya mabadiliko. Huwezi ukafanya
30
mabadiliko peke yako. Mabadiliko ni watu, na watu ni wewe na watu.
4. Jifunze kwa Wengine. Tabia ya kujifunza kwa mtumishi wa Mungu ni ya muhimu sana. Kiongozi yeyote lazima akubali kujifunza kwa watu wengine. Unapaswa kujua kwamba, kuna mtu anayekuzidi, hata kama ukiwa na karama nyingi sana, jambo ambalo unapaswa kukumbuka ni kwamba kuna mtu ambaye yuko juu yako, na huu ndio ukweli halisi. Hauwezi kuwa na kila kitu, kwa hivyo ni lazima ujifunze kwa watu wengine. Hasa jifunze kwa watu ambao wamefanikiwa. Ninajua ya kwamba suala la mafanikio lina changamoto nyingi katika tafsiri zake, kuna wengine huona mafanikio ni kuwa na watu wengi kanisani, na kuna mwingine anaona mafanikio ni kuitikia mwito wa Mungu. Mafanikio ni nini? Wacha tujibu kwa muktadha wa somo hili; mafanikio ni pale tunapoona huduma inatoka hali ya chini na kwenda hali ya juu. Mara nyingi sana katika huduma tunaangalia idadi ya watu ndani ya kanisa. Ninajua ya kwamba kuna wakati tunahitaji kuangalia hali za watu waliopo kanisani, lakini bila kujali hali zao, idadi ya watu ndani ya kanisa inaonesha kwamba kuna mafanikio. Wengine wanaangalia matoleo yanayotolewa kanisani, mfano kama kanisa hapo mwanzoni lilikuwa linaweza kutoa sadaka ya shilingi 5000 kwa mwezi, basi ikishafikia kuwa linatoa 50000 kwa mwezi, hayo yanaonekana mafanikio. Hata hivyo, wachungaji wengi hawapo tayari kushirikisha kwamba kuna matoleo kiasi gani yanatoka kila Jumapili. Na kwa sababu hiyo, unaweza kuangalia idadi ya watu ndani ya kanisa hilo. Unaweza kumtembelea kiongozi wa kanisa hilo. Unaweza kumuuliza muumini wa kawaida ndani ya kanisa hilo, unaweza 31
kuona viongozi wa kanisa hilo, na unaweza kufanya mahojiano pamoja nao. Usione aibu, hata kama ni jirani yako, acha kujitutumua, kama anakuzidi, kubali kwamba anakuzidi tu, na unapaswa uwe mpole ili uweze kujifunza. Kama huwezi kuwatembelea watu hawa, basi angalau soma vitabu mbalimbali. Kuwa mtu wa kusoma vitabu vya watu waliofanikiwa. Najua ya kwamba kiongozi anapaswa kusoma Biblia, lakini hakikisha unasoma vitabu vingine vya watu waliofanikiwa. Soma na vile vitabu vya watu ambao hawajafanikiwa. Kuna mambo ambayo utajifunza, utaona namna ambavyo wanahangaika kutoka kwenye hatua moja kwenda kwenye hatua nyingine. Suala la kujifunza halikomi mpaka unaenda kaburini. Acha kujiinua kwamba wewe una elimu ya kutosha; hata kama ukiwa na shahada ya uzamivu, unaweza kujifunza kwa mtu wa darasa la saba, na hiyo haiondoi usomi wako. Tatizo la wasomi wengi ni viburi. Usomi unaweza usikusaidie sana kwenye kuongoza mabadiliko. Na ndiyo maana unaweza kushangaa kwamba watu wanaoongoza mabadiliko, si watu wa elimu za juu sana, lakini angalau wanajifunza kwa umakini na kuwa waaminifu kwa hicho wanachojifunza. Sipingani na elimu, lakini najaribu, wasomi wakubwa kama akina Paulo walibadilisha ulimwengu, ninachojaribu kueleza ni kwamba mtu yeyote anaweza kukuzidi katika suala la kuongoza mabadiliko. Ukishajifunza kutoka kwa wengine, utakuja kugundua ni hatua gani za kuchukua, aliweza kuleta mabadiliko.
5. Kubali Kulipa Gharama Kuna gharama nyingi za kulipa kama unataka kuelekea mabadiliko ya kweli ndani ya kanisa. Na kabla ya kulipa gharama hizo, lazima kwanza upige gharama ni kiasi gani. Kama huwezi 32
kulipa gharama hizo, basi utaongoza mabadiliko kwa muda mfupi sana. Na pengine yanaweza yasiwe mabadiliko halisi. Kumbuka kwamba mabadiliko ni kitu endelevu. Siyo kwamba leo unakomaa na mabadiliko, halafu baada ya muda mfupi unaachana na dhana hiyo. Mabadiliko lazima iwe sehemu ya maisha yako. Kiongozi yeyote wa kiroho hapa duniani, ikiwa atataka kufanikiwa kuongoza mabadiliko, ni lazima kulipa gharama. Kuna gharama za aina mbalimbali za kulipa. Watu wengi wamezoea wakisikia gharama wanafikiri moja kwa moja kwamba ni fedha. Ndiyo! Fedha ni gharama mojawapo ya kulipa, lakini kuna gharama zaidi ya fedha. Kiongozi lazima ujiandae kulipa gharama zifuatazo: a) Gharama ya kihisia Nimeita kwa jina la “gharama ya kihisia” kwa sababu inagusa hisia binafsi za mtu. Gharama za kihisia ni zile tabia ambazo moyo au hisia zako zinatamani kuzifanya, na ni mambo mazuri tu; lakini kwa sababu ya nafasi uliyo nayo ndani ya kanisa, au hata serikalini inabidi uziache. Gharama hii ni kubwa sana. Nitatoa mifano kadhaa. Kama wewe umeteuliwa kuwa waziri wa wizara yoyote, kuna vitu ambavyo lazima ujinyime, ujizuie kwa sababu ya hadhi yako. Kama ulikuwa ni mchangiaji mzuri wa hoja bungeni kwa mlengo wa kukosoa serikali, huwezi kuendelea na ukosoaji huo-hizo ni gharama kwa sababu unainyima nafsi yako kile ambacho ilikizoea na ndiyo ilikuwa furaha yako. Katika mazingira hayo, hata kama ukiona serikali inafanya madudu kiasi gani, hapo lazima kunyamaza tu. Lakini hebu fikiri, kabla ya kuwa waziri, ungeweza kufoka katika vyombo vya Habari kwa kadri utakavyo. Huo ni mfano tu, ninachojaribu kusema hapa ni kwamba wewe ndiye kiongozi. Ziko tabia ambazo pengine zimesababisha huduma au 33
idara idumae kwa sababu yako. Kubali kulipa gharama za kubadilisha hisia zako. Pengine wewe ni mkali mno, na huwezi kuvumilia, sasa watu wanapokuja kanisani unawalea kama watoto wako wa kuzaa kwa sababu tu ya hisia zako. Ni lazima ukubali kuzisulubisha hisia zako msalabani. Mchungaji, au kiongozi yeyote wa kanisa kwa ngazi yoyote ile, unapokuwa umeingia katika utumishi ni lazima ukubali kulipa gharama za kihisia. Pengine ulikuwa unapenda kuvaa mavazi fulani, na hayo mavazi ni kikwazo, hivyo kwa nafasi uliyo nayo sasa huwezi kuvaa mavazi hayo kwa sababu siyo hadhi yako. Na hii ndiyo mifumo tuliyotengenezewa na jamii. Jamii ndiyo inatengeneza mifumo. Jamii ndiyo inayosema kwamba kiongozi avae suti au jeans wakati wa kuhubiri. Na huwezi kwenda kinyume na mifumo ambayo jamii imejiwekea. Kila mara huwa naawaambia watu kwamba tunavaa nguo si kwa ajili yetu binafsi, bali ni kwa ajili ya wale wanaotuangalia. Ni kwa ajili ya watu wengine. Hebu chukulia mfano, je unapokuwa chumbani mwako kwani ni lazima kuvaa nguo? Nafikiri si lazima sana. unaweza kuwa uchi wa mnyama, na hakuna mtu atakayesema chochote, lakini kama ukitoka sebuleni tu na ukute kuna hata mtoto; ama kwa hakika utatamani ardhi ipasuke uzame. Kuna watu wengi wamehama huduma kwa sababu ya mavazi fulani ya watumishi au watu wa kanisani. Ni kweli ni jambo dogo sana lakini lina maana sana. kuna mtu mwingine anaogopa kuja kanisani kwa sababu kanisa lile wanavaa nguo za gharama kubwa. Mahubiri ya mchungaji yako katika vitu vya duniani. Sasa mtu anakosa amani ya kusali kanisani hapo kwa sababu anaona mazingira yale hayamfai labda ni ya watu fulani fulani tu. Kwa sababu hiyo lazima mchungaji au kiongozi yoyote ukubali kuacha 34
vitu ambavyo unavipenda lakini vinakwaza watu. Kwa mfano katika jamii yetu ya Kitanzania, si mazoea sana kuona mchungaji anatembea na bukta (suluari fupi) barabarani. Hata kama anafanya mazoezi, watu wanatarajia kuona amevaa vizuri. Sasa kama huelewi utakuwa unapishana na watu na wanakushangaa tu. Lazima ukubali kubadilika kabla hujaanza kuongoza mabadiliko. Na ndiyo maana nimesema ni “mabadiliko yanayoumiza.” Kwa mfano kiongozi ulikuwa umezoea kwenda beach na mke wako kila weekend mnaenda kujiachia huko na minguo ya beach; huwezi kuendelea kufanya hivyo kwa sababu jamii inakuangalia na kuona mazingira kama hayo hayakufai, ni mazingira ya anasa. Jamii tayari ina picha yako mara tu unapochaguliwa kuwa kiongozi. Na ndiyo maana ukisema jambo fulani watasema “yule si fulani na ni kiongozi?” jamii imebeba tabia zako, hivyo huwezi kujitenga nayo. Lazima ukubali kwendana nayo. Kama wewe ni mke wa kiongozi, hata kama usipoingia kwenye baraza la mawaziri, au kwenye baraza la wazee wa kanisa, lakini wewe ni mke wa kiongozi, basi jamii inakuangalia kwa jicho lingine kabisa. Utasikia watu wanasema “yule si mama mchungaji?” au “yule si mke wa mbunge fulani?” mbona anavaa nguo za namna hii? Haya ni mambo ya msingi sana kuzingatia kama wewe umeshaingia katika uongozi. Hizi ni gharama za kulipa. Kihisia lazima ulipe. Nitakupa mfano mmoja katika Biblia, mtume Paulo alilipa gharama kubwa sana katika utumishi wake. Katika 1 Wakorintho 8:13 anasema “kwa hiyo chakula kikimkwaza ndugu yangu, hakika sitakula nyama hata milele, nisije nikamkwaza ndugu yangu.” Kwa namna moja ama nyingine, si nyama peke yake, kitu chochote 35
ambacho kinaweza kumkwaza mtu mwingine, basi hicho kitu hupaswi kukifanya hata kama ilikuwa sehemu ya maisha yako. Kama ni kanisani, basi anzeni kuangalia ni tabia zipi sugu ambazo zinafanya maendeleo ndani ya kanisa yasiwepo? Kuna tabia sugu ambazo watu wanaziendekeza ambazo zimekuwa sehemu ya maisha yao. Sasa hizi ni gharama za kulipa. Jiandae kwamba katika mabadiliko hayo, kuna watu ambao utawaacha nyuma na wengine wataondoka kanisani kwako kwa sababu umeanzisha vitu vipya ambavyo wao hawajavizoea. Unajua watu wanapinga sana vitu ambavyo hawajavizoea. Mara kwa mara hawakubali. Sasa kama wewe una uhakika kwamba unachokifanya ni sahihi kwa mujibu wa Biblia na umekifanyia utafiti, basi endelea. Haijalishi ni watu wangapi watabaki nyuma endelea hivyohivyo. Siku moja utaona matunda yake. b) Kulipa Gharama za Vitu Kuna vitu ambavyo wakati mwingine vinahitajika ambavyo kiongozi unahitaji kuvitoa kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kwa mfano kama mnataka kufanya kazi ya uinjilisti, viongozi wa kanisa lazima wajitolee vya kutosha kupitia vitu vyao. Katika utumishi mara nyingi ni kujitolea kwa ajili ya kazi ya Mungu. Kuna wakati unaweza ukajikuta wewe ndio unapaswa kutoa fedha ya kukodi vyombo vya muziki kwa ajili ya mkutano wa Injili, lakini kama huna hela hiyo utafanyaje? Fanya kwa kadri iwezekanavyo. Ukiwa kiongozi na huwezi kutoa vitu vyako, mali zako, basi wewe hufai kuwa kiongozi na unachelewesha maendeleo ya kanisa hilo. Kiongozi lazima uwe wa mfano. Mara nyingi watu wanapoanza 36
hata michango kanisani wanataka kujua wewe umetoa nini? Wanataka kujua kwamba umechangia kiasi gani kwenye ujenzi wa kanisa? Watu tunaowaongoza siyo kwamba ni wajinga, wanajua mambo mengi na wakati mwingine wanaamua kutuacha tu. Kwa sababu hiyo, ni lazima kwa vyovyote vile tukubali kulipa gharama za vitu. Toa vitu. Usiwe na hofu. Toa kwa moyo, na Mungu atainua huduma yako. Nimeshuhudia mchungaji akitoa kiwanja chake kwa ajili ya kujenga kanisa. Alipotoa kiwanja waumini wa kanisa waliguswa na kuanza kujitolea kwa ajili ya kujenga kanisa. Ni rahisi kusema kwamba “mchungaji huyu alikuwa na kiwanja, lakini mimi sina.” Inawezekana isiwe kiwanja, ila ukatoa kitu cha thamani kwako. Unajua thamani ya vitu inategemea. Kwa mtu mwingine kutoa kiwanja si kitu chochote kwa sababu anaweza akawa na viwanja vingi, lakini kwa mwingine kutoa hata ile shilingi mia tano anakuwa amejitolea sana. kwa sababu hiyo, toa chochote unachoweza. Huwezi kukwepa gharama ya vitu. Hata hivyo, ninao ujasiri wa kukuambia kwamba Mungu atabariki kujitoa kwako. Mungu atabariki juhudi zako kwa ajili ya ufalme wake. Hakuna mtu ambaye alitoa akaachwa. Yeyote yule ambaye alitoa kwa moyo alivuna kwa wakati wake. Hata usipovuna wewe katika maisha haya, lazima ndani ya ukoo wako watavuna matunda. Utoaji na kujitolea ni kanuni ambayo ipo kwa Wakristo na wasio Wakristo. Ndiyo maana hakuna tajiri ambaye hatoi. Jizoeze kutoa na kulipa gharama za mabadiliko.
6. Pambana na Tabia Zinarudisha Maendeleo Kuna tabia ambazo huwa zinarudisha nyuma kanisa. Tabia hizo huendekezwa na ama kiongozi mwenyewe au waumini wake. 37
Katika somo hili nazungumzia kiongozi mwenyewe na tabia zake za hovyo hovyo ambazo hurudisha nyuma maendeleo. Tabia za hovyohovyo zinaweza kusababisha kushindwa kuleta mabadiliko chanya kama hazijathibitiwa kwa ukamilifu. Hakuna mwanadamu ambaye ni mkamilifu asilimia mia moja. Katika maisha yetu tunajipima kupitia vioo vya aina mbili tu; kioo cha kwanza ni neno la Mungu. Hatuwezi kujua tabia zetu mbaya kama hazijapita kwenye kioo cha Mungu. Neno la Mungu ndilo huongoza kila kitu na kuonyesha kile ambacho kimo ndani ya moyo wako. Katika Zaburi. 119:11 tunasoma “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.” Au katika Zaburi 119:105, “Neno lako ni taa ya miguu yangu.” Neno la Mungu linapokuwa taa yako, linakuongoza katika njia zako zote, na hivyo unaweza kuona makosa yako kwa haraka zaidi kwa sababu neno linakuongoza. Mungu wetu ndiye kioo chetu. Kama ukikaa karibu na Mungu, utajihisi wewe ni mkosaji mara kwa mara na unahitaji kurekebishwa. Biblia inasema habari za Simoni Petro alikutana kwa ukaribu na Yesu kwamba “alianguka magotini pa Yesu, akisema, Ondoka kwangu, kwa kuwa mimi ni mtu mwenye dhambi, Bwana (LK. 5:8). Mara nyingi ukijiona kwamba huna dhambi, basi ujue kwamba uko mbali na Mungu. Ila ukijiona kwamba una dhambi, ujue kwamba uko karibu na Mungu wako. Hivyo jipime tabia zako mbaya zote kupitia neno la Mungu (Biblia). Kioo cha pili ambacho unapaswa utumie kujipima ni watu. Ninajua wazi kwamba si sahihi sana kujipima kupitia watu kwa sababu watu watu wanahukumu kwa kipimo cha kibinadamu. Hebu tusome Yesu alisemaje? “Ninyi mwahukumu kwa kufuata mambo ya mwili; mimi simhukumu mtu. Yohana 8:15.” Je hapa inaamaanisha kwamba hupaswa kusikiliza watu wanasemaje kuhusu 38
wewe? La hasha! Ni muhimu sana kujua watu wa nje wanasema nini juu yako. Tunapaswa kujua kwamba tunaishi katika jamii. Hapo awali nilisema kwamba jamii ndiyo huamua kwamba huyu mtu aweje, na aishije. Biblia tunayoisoma, hatuwezi kuisoma nje ya jamii. Ukisoma nje ya jamii, basi utakuwa unatangaza utamaduni wa Kiyahudi badala ya kutangaza mapenzi ya Mungu. Kwa kuwa tunaishi katika jamii, ni lazima tufike wakati tujipime kupitia jamii zetu. Usiweke pamba masikioni kuhusu maneno ya watu wa nje. Siku hizi ziko nyimbo nyingi zinazoimbwa kupuuza watu wanasema nini juu ya mtu fulani. Tena watumishi wengi hpenda kusema, hata Yesu naye alitendewa hayohayo. Unamjua Yesu wewe? Katika Luka 9:18 “Ikawa alipokuwa akisali kwa faragha, wanafunzi wake walikuwepo pamoja naye, akawauliza, je makutano wanasema ya kuwa mimi ni nani?” Si kwamba Yesu hakujua kwamba watu wanasema yeye ni nani. Yesu ni Mungu. Mungu anajua yote. Hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kufichika machoni pake. Lakini bado kwa ajili ya kuwafundisha wanafunzi wake aliuliza, je watu wanasema mimi ni nani? Unahitaji kupata watu watakaokuambia ukweli kuhusu tabia zako nzuri na mbaya. Ukipata watu wanaoweza kukuambia tabia zako mbaya, basi mshukuru Mungu. Kwa kawaida watu hawapendi kuambiwa ukweli kwa ajili ya tabia zao za asili. Unahitaji mtu wa kukuambia tabia yako ya asili ambayo inazuia mabadiliko ya kimaendeleo ndani ya kanisa. Tunazo tabia zetu za asili ambazo huwa zinaondoka polepole baada ya kumpokea Kristo. Lakini ikumbukwe kwamba hakuna mtu atakayekuwa mkamilifu mpaka siku ya kuja kwa Yesu. Na kwa sababu hiyo lazima kuendelea kujirekebisha. Watu wakikuambia habari zako, lazima uchunguze 39
kwanza, kwa sababu kuna watu wengine ambao watakuwa na lengo la kukushusha chini badala ya kukusaidia. Fanya mambo yafuatayo: Kwanza, uliza marafiki zako wa karibu kwa tabia zako nzuri ambazo zinasaidia katika kujenga huduma au kanisa liendelee mbele. Yaani hao watu wako, waambie wakwambie wazi bila unafiki tabia zipi nzuri. Kuna rafiki yangu mmoja aliniambia kwamba, “mchungaji bwana wewe ni mpole mno, yaani unatuvumilia mno, natamani ungeongeza ukali kidogo, watu wengine wanauchukulia upole wako kama udhaifu wa kushughulikia matatizo ndani ya kanisa.” Nilipoenda nyumbani nilitafakari sana ujumbe huo, lakini nikahisi kama kuna ukweli ndani yake. Lakini ilinisaidia pakubwa sana. Pili, waulize marafiki zako tabia zako mbaya ambazo wanaziona kwa wazi kabisa kwamba kwa tabia hizo huwezi kufika mahali popote. Watu wako wa karibu ni wa muhimu kukuambia habari zako mbaya kuliko wengineo. Mke au mume wako wanaweza kuwa watu wa karibu zaidi katika kukuambia ukweli. Tatu, jitafakari wewe mwenyewe. Angalia tabia zako mbaya ni zipi? Siku moja rafiki yangu mmoja aliniambia kwamba amekuwa na tabia mbaya sana ambayo hata yeye haipendi. Kwamba watu wakimpigia simu tayari ameshajua kwamba wanataka kumwambia nini, kwa hiyo anawapotezea. Sasa anashangaa wakati mwingine wanampigia na wanataka kumpa taarifa za nyumbani kwake. Hiyo nayo ni tabia mbaya kwa mtumishi wa Mungu kwa sababu lazima ujue kwamba unatumikia watu; hivyo basi ni lazima kupokea simu zao. Haijalishi ni watu wa aina gani. Acha tabia ya kumpa “mhudumu wa mlangoni” kupokea simu yako huku wewe unakunywa kahawa na mke wako ndani. Hiyo ni tabia mbaya. 40
Mabadiliko ya kweli yanapaswa kuanza na wewe mwenyewe siyo watu wengine. Nilisema hapo nyuma kwamba lazima uzisulubishe tabia mbaya. Kuna vitabia vidogovidogo ambayo inabidi uviache kabisa kwa ajili ya kuongoza mabadiliko. Kwa mfano wachungaji wengi ni wazembe. Si nyumbani na si kanisani. Yaani unakuta mchungaji ana watu thelathini tu kanisani kiburi hicho. Hawezi kukumbuka majina ya waumini wake kwa kisingizio kwamba ni wengi. Sasa kama huwezi kukumbuka majina ya watu thelathini kanisani kwako, unadhani Mungu atakuja akupe watu mia tano? Haiwezekani! Mambo mengine ni uzembe tu. Ili uweze kukumbuka majina ya watu ni lazima ujenge tabia ya kuwaombea kwa kutaja majina yao. Anza na jina la kwanza mpaka wa mwisho. Kama hukumbuki kichwani, andika kwenye karatasi na wakati wa maombi usome. Kiongozi lazima ujibu ujumbe mfupi wa maneno pale watu wako wanapokutumia. Ukishindwa kujibu ujumbe mfupi wa maneno, basi piga simu ili kujibu kile wanachouliza. Kushindwa kufanya hivyo inaonekana ni kiburi cha uzima na usifikiri kwamba wewe uko bize sana. Kuna watu wako bize, lakini wanajibu jumbe fupi kila wakati. Wachungaji wengi wengi tuna uzembe wa kutokufuatilia mipango yetu. Tunakuwa wazuri mno kupanga. Tunapanga kila kitu lakini kitu cha kushangaza ni kwamba hakuna ufuatiliaji. Unajua kwamba hakuna mtu ambaye atatenda jambo lolote pasipo kufuatiliwa. Kama mchungaji au kiongozi yeyote yule wa idara hawezi kufuatilia utekelezaji wa mipango aliyojipangia, basi ni bora akaacha kupanga mipango. Mipango ya viongozi wengi wa kanisa ipo kwenye makabrasha tu, hakuna utekelezaji wowote. Hili ni tatizo kubwa ambalo linasababisha kurudisha nyuma maendeleo ya huduma nyingi. 41
Kuna viongozi wengine ambao hawajali masuala ya muda. Watumishi wako vizuri kusema “tukutane saa sita na nusu” halafu yeye anakuja saa saba na nusu. Ni hatari sana. Kabla ya kuongoza mabadiliko yoyote ndani ya kanisa ni lazima kwanza wewe uweze kubadilika. Mkikubaliana kukutana saa saba, basi wewe kiongozi unapaswa ufike saa sita na dakika na nusu. Hoja yangu hapa kwamba wewe kama kiongozi unapaswa kuwa ndani ya wakati na si nje ya wakati. Kama ukizoea tabia ya kuchelewa kila wakati, basi ujue kwamba tabia hiyo itakuja kukugharimu siku moja.
7. Kuwa Sauti ya Matumaini na Maono Kiongozi akisema “hapa tunaweza” watu wengine wote wanatafuata. Kiongozi akisema, “hapa hatuwezi kupita,” watu wote watafuata. Kiongozi ni sauti ya matumaini. Kiongozi anapaswa kuwa ni mtu mwenye sauti ya matumaini. Sauti ya matumaini ni sauti ambayo imejaa maono ndani yake. Kama kiongozi akiwa na maono, atakuwa anaona kila kitu mbele yake kinawezekana. Vitu ambavyo haviwezekani havitaonekana mbele yake kwa sababu anaamini kwamba kila kitu anachokifanya Mungu amekibariki. Unajua Mungu anatafuta watu wenye imani na sauti ya matumaini kwa watu wengine ili aweze kuwatumia. Kama kiongozi anaona giza mbele, basi waumini wa kawaida wataona giza totoro mbele yake. Kuna mchungaji mmoja aliwahi kusema kiongozi anapaswa anapotembea mbele anaona mbali sana, na akiangalia nyuma akute watu wanamfuata. Akute watu wanasema huyu atatufikisha tunakoelekea. Yeye mwenyewe ana sauti ya matumaini. Kama usipokuwa sauti ya matumaini kwa wale wanaokufuata, basi wewe utabaki mtu wa kulaumu tu.
42
Kanisani kwako ni lazima kila mtu ajue maono ya kanisa ni nini. Kuna wachungaji wengine siku hizi wanaweka bango kubwa ndani ya kanisa na wanaandika maono ya kanisa hilo kwa ujumla. Kanisa linapokuwa na maono ya wazi yanasaidia watu wengine kujiunga katika kutekeleza maono hayo. Maono siyo ya kuweka mfukoni. Maono siyo ya kwenye makaratasi. Maoni ni ya kupeleka kwa watu. Unapokuwa na maono, halafu hutaki kuwashirikisha waumini wako, basi ujue kwamba hayo maono kamwe hayatakuja kutimia. Ukiwashirikisha watu maono, wanajiamini na kujiona kuwa sehemu ya utekelezaji wa maono hayo. Ukijitahidi wewe peke yako kutekeleza maono hayo, basi ujue kwamba watu wengine unawaacha, na hawatashiriki katika utekelezaji wa maono hayo. Sifa za Kiongozi mwenye Sauti ya Matumaini Nitajaribu kuelezea mambo ya msingi ambayo yanaweza kumfanya mtu akawa sauti ya matumaini kwa watu anaowaongoza: a) Ni Mtu anayesoma Neno la Mungu kwa Bidii Hakuna hekima zaidi ya ile inayotoka kwa Mungu. Mungu huzungumza nasi kupitia neno lake. Unaposoma neno la Mungu (Biblia), maana yake Mungu anazungumza na wewe. Unapoomba, maana yake wewe unazungumza kwa Mungu. Ukisoma na kusikiliza neno la Mungu unapata maongozi ya kiroho. Biblia inasema katika Wakolosai 3:16 kuwa “neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu."Pia Mungu alimwambia Joshua kwamba "kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapostawi sana” (Joshua 1:8). Katika mstari huu tunajifunza mambo yafuatayo: 43
a) Ili uweze kufanikiwa katika mipango yako ni lazima kitabu cha Torati kisiondoke kichwani mwako. Maana yake wewe uwe unalikumbuka neno la Mungu katika kila maamuzi unayotaka kuyafanya katika maisha yako. b) Ili uweze kufanikiwa unahitaji kutafakari neno la Mungu. Kwamba kabla hujafanya jambo lolote la kimaamuzi, lazima kwanza utafakari neno la Mungu. Kutafakari maana yake ni kulifikiria neno la Mungu na jinsi ambavyo linakukambia kufanya na ufanye c) Tendo la kushika neno la Mungu ni la ziku zote (usiku na mchana). Usishike neno la Mungu tu pale unapokuwa na uhitaji, bali ni wakati wote. Tatizo la watu wengi ni kwamba wanapenda kuamua mambo yao kwa kutegemea ndoto. Hawataki kusoma neno la Mungu kwa sababu wanadhani linawachelewesha kufanikiwa. Lakini wacha nikwambie mtu wa Mungu kwamba, kwa kuwa umeamua kuiendea njia ya kweli ya Kimungu, na kwamba unayo nia ya dhati ya kuongoza mabadiliko katika kanisa lako, basi hauna njia nyingine zaidi ya kusoma au kusikiliza neno la Mungu na kulitendea kazi. Ndoto zinaweza kubadilika badilika, lakini neno la Mungu limejaa ahadi nyingi ambazo ukizisoma zinakutia moyo wa kuendelea. Kila changamoto unayoipitia katika huduma, inayo majibu kutoka kwenye Biblia. Kwa hiyo ni lazima kusoma neno la Mungu. Viongozi walioleta mapinduzi katika Ukristo kama akina Martin Luther, John Calvin na wengineo walikuwa ni watu wa kusoma neno la Mungu. Martin Luther inadaiwa aliweza kukariri kitabu cha Warumi chote. John Calvin aliandika commentary (mafafanuzi) katika vitabu vyote vya Biblia isipokuwa Ufunuo wa 44
Yohana. Unaweza kuona namna watu hawa wamejibidisha katika kusoma neno la Mungu.
walivyokuwa
Siku hizi urahisi wa kusoma neno la Mungu umeongozwa. Unaweza kuwa na Biblia kwenye simu yako. Zipo Biblia ambazo zinaaminika kwenye simu na unaweza kuzipakua na kusoma kila siku. Si tu hivyo, bali unaweza hata kusikiliza kwa sauti. Nimejijengea tabia moja kwamba kabla ya kulala, ninaweka sauti ya Biblia ili nikipata usingiza, basi nipate usingizi mtamu huku nikitafakari neno la Mungu. Kwa vyovyote vile katika kipindi hiki hakuna udhuru kabisa. Ni lazima uwe mtu wa neno la Mungu ili uweze kuongoza mabadiliko yanayoumiza. Neno la Mungu kwako liwe ndiyo chanzo cha maarifa yote. Unaweza kusoma vitabu vingine lakini mkazo mkubwa uwe kwenye neno la Mungu. b) Ni mtu mvumilivu Kama unataka kufika mbali kwenye huduma unayoingoza, basi jitahidi sana kuwa mvumilivu. Uvumilivu ni mojawapo ya tunda la Roho. Unapokuwa mvumilivu, itakufanya wewe uweze kuamua mambo yako vizuri zaidi kwa utulivu. Kiongozi mwenye maono, huambatana na uvumilivu na hutaka kujaribu vitu vipya, kupata fursa mpya na anajua jinsi ya kubaki kwenye lengo lake kwa uvumilivu wote. Siyo kiongozi unapigwa majungu wiki moja tu unajiudhuru. Kuna watu wengi wanapenda kusema kwamba kujiudhuru ni hekima. Lakini mimi huwa nasema “kujiudhuru ni hekima kama nimekosa” lakini kama sijakosa, siwezi kujiudhuru. Kujiudhuru kwa sababu eti watu wamekupiga majungu hakuwezi kuleta maendeleo yoyote katika huduma yako. Kuna viongozi wengi 45
kanisani wanachaguliwa kwa kura nyingi lakini wakipigwa majungu tu wanaacha kazi. Tatizo kubwa kanisani ni kwamba watu wanaona kazi ya Mungu ni kazi ya kujitolea, na kwa sababu hiyo hawaoni umuhimu wa kuvumilia zaidi. Na ndiyo maana ukipigwa jungu moja tu, unahamia kanisa lingine, ukifika huko nako wanakupiga majungu, unahamia kanisa lingine, unakuwa unahama hivyohivyo, mpaka unakufa watu hawajui wewe ni muumini wa kanisa gani. Wewe unayo talenti ya uongozi, lakini bila kuwa mvumilivu, huwezi kufika mbali. Jivike uvumilivu mtu wa Mungu utafika mbali sana. Watumishi wa Mungu wote walioendelea kihuduma wote hawa walikuwa wavumilivu. Unakuta huduma imekuwepo mahali kwa muda wa zaidi ya miaka ishirini lakini hakuna kitu kinachoendelea hapo hata kidogo. Lakini unaona mchungaji anaendelea kusimama vizuri na anatimiza wajibu wake. Katika uvumilivu pia tusisahau kwamba tunahitaji kutumiza wajibu wetu. Kama hutimizi wajibu wako na unavumilia, haisaidii chochote bali unajisumbua tu. Katika kila eneo jivike uvumilivu wa hali ya juu, utaona matokeo ya uvumilivu. Katika uvumilivu lazima hekima iwepo. Usivumilie hovyo. Kwa mfano kama ni suala la ukuaji wa huduma, jambo la kwanza unapovumilia hakikisha uko eneo sahihi. Kuna watu wengi wanaanzisha huduma katika maeneo magumu, halafu wanajitia moyo kwa uvumilivu. Usijaribu kuvumilia bila kufikiri. Nitakupa mfano katika maisha ya utumishi wa Paulo. Katika kitabu cha Matendo ya Mitume 18:6 Biblia inasema “Walipombishia na kumtukana alikung’uta mavazi yake akawaambia, Mimi sina lawama, mkipotea, lawama iko juu yenu wenyewe. Tangu sasa 46
nitawahubiria mataifa neno la Mungu.” Ukiangalia mahali hapa utagundua kwamba Paulo alikuwa na nia ya kuwahubiri watu Wayahudi. Alijitahidi sana kuwaunganisha, lakini kwa kuwa Wayahudi walikataa, basi Paulo akasema isiwe tabu, akageukia kwa watu wa Mataifa. Hii inamaanisha kwamba watu wa kwanza ambao Paulo alitaka kuwahubiria walikuwa ni Wayahudi, lakini kwa kuwa walikataa aligeukia watu wa mataifa.
c) Ni Mtu wa Mikakati Kiongozi yeyote anayejielewa, na mwenye kuleta mabadiliko makubwa, ni mtu mwenye mipango ya kimkakati. Kupanga kimkakati ni ustadi ambao viongozi wengi wa maono wamekuwa wakifanya. Viongozi wa namna hii wanaweza kufikiria wanachotaka siku zijazo zionekane, na kisha kupanga mikakati ya jinsi ya kufika hapo. Kuwa sauti ya matumaini maana yake ni kuwa mtu wa mikakati. Kiongozi anapewa idara hajapanga mkakati wowote hawezi kuendelea hata kidogo. Unapopanga mkakati lazima mkakati huo uwe na mbinu ambazo zitawezesha kufika kwenye lengo hilo. Unapokuwa ni mtu wa mikakati inakuwa ni rahisi kwako kujieleza hata baada ya uongozi wake. Tunazo changamoto nyingi kwenye makanisa yetu kwamba mtu anachaguliwa kuwa kiongozi wa ngazi ya juu kabisa lakini hana mikakati wowote. Ni mtu wa maneno tu. Unajua siku hizi hata makanisani watu wanataka wachungaji wenye mikakati. Wanakwambia kwamba kama wewe ni mchungaji wa kuhubiri tu, basi sisi tunao wengi sana wanaoweza kuhubiri. Sasa hivi ukikabidhiwa kanisa, ni kama mtu amekabidhiwa 47
kampuni. Watu hawataki kusikia kwamba kanisa linashuka. Sasa basi ukiwa ni mtu mwenye mipango na mikakati mizuri, unaweza kufanya vizuri zaidi. Kuwa mtu mwenye mikakati ili uweze kuongoza vizuri mabadiliko ndani ya kanisa lako.
8. Tarajia Upinzani Kwenye Mabadiliko Watumishi wa Mungu wengi hupenda kusema, “nina imani kubwa, hakuna kitu kinachoweza kunirudisha nyuma.” Ha! Ni kweli, kama unayo imani kama hii uko vizuri, lakini nataka nikuambie kwamba mbele yako kuna upinzani mkubwa sana katika kile unachokifanya. Upinzani kwenye suala linaloleta mabadiliko ni jambo la kawaida kabisa. Kuna watu ambao wanapenda mabadiliko, wengine wanapenda kuona mabadiliko yakitokea lakini hawataki kuwa sehemu ya mabadiliko, huku wengine wakiwa katikati. Kundi ambalo linaweza kukupinga kwa nguvu zaidi ni lile ambalo halitaki mabadiliko. Kundi hili tumejifunza kuwa ni wale watu ambao wamesharidhika na hali ya kanisani. Yaani kwao hawana shida yoyote, wameridhika kuona idadi ndogo ya waumini, wameridhika kuona kila kitu kiko vilevile. Sasa basi unapaswa kujiandaa na utarajie upinzani. Jinsi Ya Kushughulikia Upinzani Yamkini umekwisha kujifunza namna ambavyo unaweza kushughulikia upinzani ndani ya kanisa, hata hivyo ningependa kusema kwamba kuna upinzani mwingine ambao ni mzuri kwa namna fulani kwa sababu hukuimarisha wewe katika uongozi wako; hata hivyo upinzani ambao unaona ni hatarishi kwa huduma ni lazima ujue namna ambavyo utashughulikia. Sisi kama Wakristo, hatushughulikii upinzani ndani ya kanisa kwa kuwafukuza watu 48
ambao wanaonekana kukupinga. Kama ukiwafukuza watu wanaokupinga, kamwe utamaliza kanisa zima, kwani baada ya kuwafukuza hao, lazima kundi lingine litatokea kupinga kile unachofanya. Sasa basi ili uweze kuzima upinzani unahitaji kupata maarifa yafuatayo: a) Elewa asili ya upinzani huo Sisi watu wa nuruni, hatupaswi kukurupuka katika kutatua masuala matatizo ndani ya kanisa. Tunahitaji hekima ya peke yake katika kutatua changamoto hizi. Inawezekana wewe siyo mchungaji, lakini ni kiongozi wa kanisa; basi hata kama siyo mchungaji, ni lazima ujifunze roho ya uchungaji ya kushughulikia matatizo. Kitu cha kwanza kabisa unapokuwa umebaini upinzani katika huduma yako ni kujua asili ya upinzani huo. Jiulize maswali yafuatayo ili yakusaidie kujua asili ya upinzani; Kwa nini watu wanapinga hiki ambacho nataka kukifanya ndani ya kanisa? kuna watu wangapi ambao wanapinga? Kuna watu wangapi nyuma yao? Je wana ushawishi kiasi gani? Je nikiwasikiliza kuna madhara gani yanaweza kutokea? Je nisipowasikiliza kuna chochote kinaweza kutokea? Je wako katika kundi gani la watu ambao tumewazungumzia kule nyuma? Nini hasa kusudi la kupinga? Je wako sahihi au hawako sahihi? Kwa kweli unahitaji kujua kabisa asili ya upinzani huo. Mara nyingi sana watu huinua upinzani katika maendeleo kwa sababu zifuatazo: i.
Masilahi binafsi
Watu wengine hupinga mabadiliko kwa sababu ya maslahi binafsi, yaani anaamini anaweza kupoteza kitu muhimu kutokana na 49
mabadiliko hayo, basi kuna uwezekano wa kupinga mabadiliko hayo. Watu wengine ndani ya kanisa huzingatia masilahi yao; kwa mfano heshima waliyo nayo, pamoja na mambo mengine mengi. Mtu mmoja alinisimulia kwamba alitaka kufanya mabadiliko makubwa ya utoaji ndani ya kanisa, kwa sababu kila mwezi alikuwa anaona sadaka ni zilezile na watoa zaka ni walewale. aliwaita viongozi wa kanisa ili kujadili mbinu za kuongeza kiwango cha utoaji, na walinza na utoaji wa zaka. Kila mmoja alipendekeza njia ambayo inaweza kusaidia watu kutoa zaka. Hata hivyo njia ambazo zilikuwa zinapendekezwa zilionekana kutumiwa mara zote na hapakuwa na mabadiliko yoyote, hivyo basi mchungaji alipendekeza kwamba kila Jumapili wasome majina ya watoa zaka; kwa kwa kuanza na viongozi kwanza. Mtumishi huyu anasema, “viongozi karibu wote walipinga wazo hili, huku wengine wakielezea matarajio yao kwamba kusoma majina ya watu si vizuri. Lakini mwishoni nilikuja kugundua kwamba hawa viongozi wanaona aibu kwa sababu ya heshima zao ndani ya kanisa, na kwa kuwa walikuwa hawatoi, wasingekubali kuunga mkono mabadiliko hayo. Sasa nini kiliendelea, wacha iwe siri yangu.” Sasa viongozi wa aina hii lazima watakuwa wanapinga mabadiliko. Kutatua hili ni kwamba wanahitaji kuambiwa wazi kwamba wanahitaji kutoa zaka. ii.
Tathmini Tofauti
Wengine wanaweza kupinga mabadiliko kwa sababu ya tathmini tofauti. Hawaoni umuhimu wa mabadiliko hayo kwa sababu pengine labda hawakuamini wewe kama unaweza ukaongoza mabadiliko hayo. Sasa wakitathmini wanagundua na kuona kwamba huwezi kuwafikisha popote, basi huamua kupinga kabisa. Kwa mfano kuna viongozi ambao wana mipango mingi sana, lakini 50
hakuna mpango hata mmoja ambao umewahi kutekelezwa katika uongozi wao. b) Weka Wazi Mabadiliko Unayotaka Wakati mwingine watu wanaweza kupinga kwa sababu hawaelewi hata mabadiliko unayotaka kuyafanya kanisani. Eleza sababu za kutaka mabadiliko ndani ya kanisa. Kwa mfano kama wewe ni mwenyekiti wa kwaya, na unahitaji mabadiliko kwenye kwaya, basi weka wazi unataka mabadiliko yapi? Je hayo mabadiliko yanafikika? Katika kuweka wazi hakikisha unaweka malengo yenye changamoto, yanayoweza kufikiwa na ya kuvutia. Kuwa wazi katika mwongozo kuhusu malengo. Watu watakapoona kwamba umeweka wazi; hatua kwa hatua, hata kama ni mabadiliko magumu sana, wataona ni kawaida kwa sababu unafanya kidogo kidogo. Usijaribu kufanya kila kitu kwa siku moja au kwa wiki moja au kwa mwaka mmoja. Weka wazi malengo hayo, na kama utaweka wazi unaweza kujikuta kwamba hawa watu wanaelewa zaidi na kukubaliana na kile unachokifanya. Kitu ambacho mchungaji unaweza kukifanya bila kushirikisha viongozi wa kanisa ni kuandaa mahubiri yako ya Jumapili. Kwenye mahubiri unayo mamlaka makubwa sana, lakini linapokuja suala la uongozi, watu ulionao sio watoto, wanataka kujua unafanya nini, wanataka kujua una mipango gani ya baadaye, wanataka kuona wakishirikishwa. Kwa hiyo epuka kuandaa mipango yako ukiwa chumbani kwako, halafu utarajie kwamba watu watakwenda kuipokea, uongozi wa namna hiyo ni wa kibabe, na wala siyo wa kibiblia. Usiogope kwamba utakapowashirikisha watakupinga. Je utajuaje kwamba hawa watu wanakupinga kama haujawahi kuweka 51
wazi mipango yako. Ni lazima kuwaonyesha wazi mipango yako, na unataka mabadiliko ya aina gani, na utatumia mbinu zipi katika kufikia mabadiliko hayo, na kwa jinsi gani umejiandaa kukabiliana na changamoto. Haya ni mambo ya msingi kwa kiongozi ili uweze kuepuka majungu na upinzani katika uongozi wako. c) Epuka kupanga mipango ya mabadiliko chumbani kwako; na kisha unataka watu watelekeze Kwakweli viongozi wengi huwa wanapata majaribu ya kupanga mipango wakiwa majumbani kwao na wakati mwingine hata hawafanyi maombi maalumu, na wakati mwingine hata bila kuwashirikisha viongozi wa kanisa. Sasa inapotokea kwamba unataka viongozi wengine waweze kutekeleza mpango huo, mara nyingi utakumbana na upinzani mkubwa. Wakati mwingine unaweza kuona watu hao kama wana pepo, lakini ukweli ni kwamba hauja washirikisha. Kwa hiyo, tunapaswa kuwashirikisha watu mipango yote (hasa wale viongozi). Tukishindwa kuwashirikisha basi tutaona kuwa ni wapinzani wetu. Katika kumalizia hoja hii ya kujiandaa kukabiliana na upinzani, ningependa kusema kwamba, usijidanganye kwamba upinzani haupo. Wapinzani wa kanisa siyo maadui zako bali ni ndugu ambao unapaswa kuwalea na kuwaongoza kama kaka na dada katika Kristo. Yawezekana wapinzani wako sahihi. Usiwe na dhana kwamba kila anayekupinga ni adui yako. Kuna watu wanapinga mipango yako kwa sababu hawaoni mwelekeo vizuri. Kubali kukabiliana na upinzani. (kumbuka; upinzani ninaozungumzia sio ule wa vyama vya upinzani)
52
9. Shughulika na Mahitaji ya Watu Mtumishi wa Mungu yeyote ameitwa kwa ajili ya kushughulika na mahitaji ya watu kanisani au popote pale. Rais anapoteua mawaziri, anataka wamsaidie katika kutatua mahitaji ya watu. Hakuna ajenda nyingine zaidi ya kutatua matatizo ya watu. Kama kiongozi hawezi kutatua matatizo ya watu, basi huyu hajui nini maana ya uongozi. Unahitaji kujua kwamba unaongoza mabadiliko ndani ya kanisa kwa sababu unataka kutatua mahitaji ya watu. Kabla ya kujua namna ambavyo unatatua matatizo ya watu, jiulize kwanza, kwa nini nimefanyika kuwa kiongozi? Hoja kubwa ya kiongozi ni kutatua matatizo ya watu. Popote pale duniani matatizo hayajawahi kuisha. Duniani pote kuna matatizo. Unafikiri kwa nini kuna matatizo duniani pote? a) Kwa sababu ya dhambi (Mwanzo 3 inaeleza chanzo cha dhambi) na dhambi hiyo ilienea duniani kote. b) Watu ni walewale. Ni rahisi sana kusema kwamba mimi ni maskini, fulani ni tajiri, kwa sababu hiyo hata shida. Watu wote duniani wanatofauti ndogo ndogo tu, lakini watu ni walewale. c) Watu wote wameathiriwa na matokeo ya dhambi. Kifo kikiwa kinaongoza katika kuhakikisha kwamba mwanadamu haishi kwa amani hapa duniani. Watu wengi wanaishi kwa hofu ya kifo. Wanaogopa kufa. Hata ukikuta wakristo wanaimba nyimbo kwamba wanatamani kwenda kuishi na Baba mbinguni, hawako tayari kwenda kwa wakati wakiwa wanaimba. Kwa sababu hiyo tatizo lipo.
53
Kwa kuwa matatizo ni mengi duniani, lazima kiongozi ajue kwamba anaingia katika uongozi kwa ajili ya kutatua tatizo la watu. Kama nilivyobainisha hapo juu kwamba mwanadamu ametenda dhambi. Biblia inasema kwamba “wote wamefanya dhambi na kupungukiwa na utukufu wa Mungu” (Warumi 3:23). Kazi ya kiongozi wa kanisa ni kutengeneza mazingira ya wenye dhambi kuingia kanisani ili waokolewe. Ni kuwafuata wenye dhambi popote pale walipo ili aweze kuwaleta kwa Kristo. Hapo ndipo utakuwa unatatua matatizo ya watu. Watu wanapokuwa wamekuja kanisani wanatakiwa wasikie ujumbe wa matumaini katika maisha yao kwa kuhakikishiwa kwamba wamesamehewa dhambi zao kabisa. Kiongozi popote pale alipo, anapaswa kufikiri namna ambavyo anaenda kushughulikia matatizo ya watu wa kanisani kwake. Watu wa jamii yake. Makundi mbalimbali ya watu. Wewe umeitwa kuwa sauti ya matumaini na maono. Popote pale ulipo, watu wanapaswa wajisikie uwepo wako. Kiongozi wa kanisa anapokuwa ametembelea hata familia ya muumini, ni lazima ile familia iseme “kweli Mungu ameonekana kwetu” kwa sababu wewe ni kiongozi wa watu na unataka kushughulikia matatizo ya watu. Katika kushughulikia matatizo ya watu ni pamoja na kuwasaidia kwa mambo mbalimbali. Nataka niweke hapa njia bora ya kushughulikia mahitaji ya watu.
Njia Bora za Kushughulikia Mahitaji ya Watu Kuna njia mbambali za kuonyesha kwamba unajali watu. Hauhitaji kuwa na mali nyingi ndipo uoneshe kwamba unawajali na kushughulikia matatizo yao. Hauhitaji kugawa hela mtaani ndipo uonekane kwamba unawajali watu. Unaweza kufanya jambo dogo na likaonekana kubwa sana mbele ya watu wengine. 54
Unahitaji kuwapenda watu wako. Wapende kutoka moyoni mwako. Hebu tujiulize swali hapa, je upendo nini? Kuna tafsiri nyingi sana za upendo. Ila mimi katika sehemu hii wacha nitafsiri kwamba upendo ni “kujali.” Kwamba unamjali mtu bila shuruti ya kitu kutoka ndani. Mungu wetu alitujali sisi kwa hiyo alitupenda. Biblia inasema kwamba “sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza. (1 Yoh. 4:19). Pia anasema “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na Uzima wa milele.” (Yoh. 3:16). Yohana ametuonyesha moja wapo ya tabia ya upendo kwamba ni “kujali.” Kujali kwa kutoa. Mungu alitujali, na kwa sababu hiyo alimtoa mwanawe Yesu Kristo kwa ajili yetu. Kama mtu unamjali unaweza kutoa. Kuna vitu vingi vya kutoa kama unajali; kwa mfano unaweza kutoa muda wako kwa ajili ya yule unayempenda: kukaa naye, kuzungumza naye, kumshauri, kumwombea, kumtia moyo, pamoja na mengineyo mengi. Huo ndio upendo ambao mimi nauzungumzia hapa. Kiongozi anahitaji kuwapenda anaowaongoza bila kujali matabaka yao. Watu wako katika matabaka ya aina mbalimbali; kuna wengine maskini, wengine matajiri, wengine wasomi na wengine siyo, wengine wana vyeo vikubwa serikalini, na wengine hawana vyeo vyovyote. Hawa watu wote wanaishi katika jamii moja. Katika jamii hakuna cha mtu mwenye sifa bora kuliko mwenzake. Nilisema hapo awali kwamba jamii ndiyo inatengeneza sifa za watu, namna wanapaswa wafanye, lakini linapokuja suala la upendo, kiongozi lazima uwapende watu sawasawa. Kuwapenda wale unaowaongoza kunaonesha kwamba wewe unajali hali zao. Kama hutaki kuwapenda basi usiwe kiongozi wao. Huwezi kuongoza mabadiliko yoyote kama huna upendo wa dhati 55
kwa wale unaowaongoza. Kuna tuhuma kwa watu viongozi wengi kupendelea watu wenye vyeo au matajiri kanisani kwa sababu wanawapatia vitu fulanifulani; ubaguzi wa namna hii haumtukuzi Mungu. Ukianza kuwapenda kwa matabaka, mwisho utakisikia “kiongozi fulani tumemweka mfukoni, hawezi kusema lolote.” Tunapokuja kwenye eneo la kanisani sasa, kiongozi yeyote lazima apende kundi lake kwa kuwajali na kuwahesabu kama watu wanaomhitaji yeye kuliko mtu mwingine. Kujali mahitaji yao kwa upendo kabisa. Onesha wazi kwamba unawapenda, na kwamba unataka waendelee kukua kimwili na kiroho pia. Usijaribu kuonyesha matabaka ya aina yoyote katika uongozi wako. Wapende wote kwa usawa na uwatendee yote yanayofaa. Tumia muda wako kwa ajili yao; kwa mfano unaweza kupanga muda wa kuzungumza nao hata kwenye vikundi mbalimbali wanapokuwepo kanisani. Kama wewe ni mchungaji, kazi kubwa ni kuwatembelea pia kwa upendo na kuweza kusikiliza shida zao na kuzipeleka mbele za Mungu. Si kwamba wao hawawezi kuomba! Hapana, bali unapoomba pamoja nao unaonesha kwamba unawajali. Kumekuwepo na changamoto ya wachungaji wengi kuhesabu waumini kanisani tu, bila kujua wanaotokea wapi. Ni kweli si rahisi kujua kama kanisa ni kubwa sana, lakini wachungaji wasaidizi lazima waoneshe upendo wa karibu kwa watu. Kuna watu wengine tukienda majumbani kwao tutajifunza kitu na tutazidi kuwahudumia zaidi na zaidi. Inawezekana huna vitu vya kutoa kwa watu, lakini unaweza ukachukua hata sabuni tu. Unajua sabuni ambayo inatoka kwa mchungaji ni ya thamani kubwa sana kwa muumini. Muumini anajiona kwamba kumbe “kiongozi wangu ananipenda.” Unaweza kushangaa kwamba sabuni hiyo hawawezi hata kuitumia na badala yake wakaiweka mezani tu iwe ukumbusho 56
kwao kwa sababu si jambo la kawaida kwa watumishi kupenda kwa kutoa vitu. Watumishi wengi wamezoea kupokea tu kutoka kwa waumini, huku wakiwa na ujasiri wa kufundisha kwamba “ni heri kutoa kuliko kupokea.” Kama wewe ni kiongozi kanisani; kwa mfano mzee, shemasi, kiongozi wa idara, jitahidi ujali watu walio chini yako. Inawezekana kwamba ukawa na mambo mengi ya kufanya; kila siku unaondoka kwenda kazini kuanzia asubuhi mpaka jioni. Unarudi ukiwa umechoka sana na hutamani hata kidogo kufanya kazi yoyote. Wewe ni mwanadamu, kama walivyo wanadamu wengine. Lakini siku hizi tunazo simu. Asilimia kubwa ya watu kanisani wanazo simu za kawaida, hivyo basi unaweza angalau kutuma hata ujumbe mfupi wa maneno kwa muumini. Wengi tumekuwa tukijiunga na vifurushi mbalimbali vya mitandao, lakini jambo la ajabu ni kwamba vinamaliza muda wake bila hata kupiga simu au kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa wapendwa wetu. Tafuta muda angalau hata dakika moja utume ujumbe. Mpendwa mwenzio akipokea ujumbe atabarikiwa, atafurahi, atajengwa, atahuishwa hata kama alikuwa amekata tamaa. Ukisikia mpendwa akiwa katika changamoto, jaribu kushughulikia changamoto hiyo kwa uharaka zaidi. Si lazima utoe kitu chochote, lakini kule kujali na kuomba kwa ajili ya jambo lake kuna saidia mtu huyu hata kama alikuwa amekataa tamaa anainuka. Najua kwamba wachungaji wengi wanajua namna ya kuwahudumia waumini wao, lakini hapa narudia kusema kwa ajili ya msisitizo kwamba tunahitaji kuwajali watu wetu kwa kuwapenda sawasawa (equally). Hivyo basi, kama kiongozi, unahitaji kuwajali watu bila kuwagawa, huku ndiko kushughulika na matatizo ya watu. 57
10. Kuthamini Watu Wanaokuunga Mkono Hoja hii haipo kwa ajili ya kuweka makundi ndani ya kanisa. Pia haipo kwa ajili ya kuleta upendeleo kwa watu wengine kanisani. Hata hivyo ninachojaribu kusema hapa ni kwamba watu wengi katika kanisa lako hawatapinga mabadiliko hayo na watafuata mwongozo wa viongozi ambao wanaunga mkono mabadiliko hayo, lakini usiwachukulie kawaida. Thom Ranier anasema kuna makundi matatu vya watu katika kanisa lako: watu ambao wako tayari kubadilika, watu wanaofuata wengine, na watu ambao ni sugu. Ni kawaida kuzingatia watu wanaopinga mabadiliko, lakini kumbuka wao ni wachache, hibyo weka umakini wako kwa wengi ambao wanataka kusonga mbele, na panga kuwasiliana na kusambaza mabadiliko kwa njia nzuri, kwa wakati unaofaa. Mpango wako wa kuwasiliana nao mabadiliko unapaswa kuzingatia hatua zinginezo tulizojifunza hapo juu. Kama kiongozi, jitahidi watu ambao wanakuunga mkono kuwapongeza na kuwashukuru sana katika kufanya kazi pamoja nao. Kama kiongozi wa kanisa, ni rahisi kusahau kuwa watu wengi unaofanya nao kazi ni wa kujitolea. Watu wengi husahau suala hili, na wakati wanapoanza kuongoza mabadiliko wanaanza kutumia mabavu kana kwamba wanawalipa watu hao kwa muda wao. Hawa watu wanajitolea tu. Wanatoa muda wao, mali zao, nguvu zao kwa ajili ya upendo wao kwa Mungu. Kama wao, unapaswa kutoa shukrani na kupongeza kwa wazi wale wanaoshiriki katika mabadiliko. Unaweza kutuma barua pepe, ujumbe mfupi wa maandishi, au barua kama njia ya kuonyesha shukrani yako kwao, pia. Ukifanya hivi unaweza kujenga mazoea mazuri na watu hawa watajisikia kuwa sehemu ya mabadiliko, na pia wataona kwamba
58
unawajali. Kila mtu anapaswa ajisikie kwamba kiongozi ananijali kuliko watu wengine; ni kazi yako kumfanya ajisikie hivyo. Kwa mfano kama kulikuwa na tukio kanisani, viongozi wa kanisa wamefanya vizuri katika kuunganisha nguvu zao; wewe kama mchungaji tafuta nafasi ya kuwapongeza. Hata kwa ujumbe mfupi wa simu kwamba, “kwa kweli leo umefanya kazi vizuri.” Nakwambia kwamba ujumbe huo hataufuta huyo ndugu, ataguswa sana. Lakini ukichukulia poa tu kwamba lazima wafanye, basi utakuwa unawakatisha tamaa. Siyo mtu mmojammoja peke yake, pia kanisa kwa ujumla, washirika wanahitaji kutiwa moyo na kupongezwa katika ushiriki wao mzuri katika kazi ya Mungu. Kazi ya mchungaji kubwa ni kuhakikisha kwamba unawasababisha washirika wote wakuunge mkono, hivyo basi kupitia shukrani zako na pongezi, inaweza kuwa daraja zuri kwa ajili ya kuwaunganisha na kuwa kitu kimoja.
11. Kubali bila Majuto wengine Waondoke Pale unapoona kwamba wengi huwa na kukubali wazo lako la kuleta mabadiliko, unapaswa pia kujua kwamba sio wote wataunga mkono mabadiliko yako. Na kwa sababu hiyo, unahitaji kuwaacha wengine waondoke kanisani, ikiwa hawatakubaliana na mabadiliko. Sisemi kwamba ufukuze watu kanisani, bali nasema kama mabadiliko hayo ni ya msingi kabisa, na watu wachache sana wanapinga, basi unahitaji kuwa kuwaruhusu waondoke au waamue kubaki wenyewe. Nilisoma habari ya mchungaji mmoja, ambaye aliongoza mabadiliko katika kanisa la lake. Alipokuwa katika kuongoza mabadiliko hayo, kanisa lilikuwa na waumini 50, lakini baada ya kuongoza mabadiliko makubwa ya kufanya uinjilisti nyumba kwa 59
nyumba, mtu kwa mtu, rafiki kwa rafiki; baadhi ya watu walipinga mwamko huo, na badala yake walihama kanisa. Baada ya mwaka mmoja, kanisa hilo liliongezeka na kuwa na watu 80. Mchungaji alipoulizwa kwamba amefanyaje ili kuongoza waumini ndani ya kanisa kufikia mabadiliko hayo alijibu kwamba "nilifanya mabadiliko makubwa sana, kwanza niliondoa idara ya Uinjilisti ikawa idara ya kanisa zima, nilibadilisha viongozi kadha wa kadha, lakini nasikitika sana kwa sababu katika mabadiliko hayo, nilipoteza waumini watano." mchungaji aliyekuwa anauliza maswali haya, alishangaa sana jibu kutoka kwa mchungaji, yaani wewe umepoteza watu watano tu na unalalamika? Alisema, “Hata ungepoteza 20 halafu ukawapata 30 zaidi, bado ungebaki na 10. Maana ya mfano huu, si kwamba tudharau watu wengine au kwamba tukatae kupokea maoni ya watu wengine, bali ni kwamba, unapoona kwamba mabadiliko unayofanya yataleta faida kubwa; basi inabidi ukubali wengine kuondoka. Ninasisitiza ukubali bila majuto, kwa maana ya kwamba usije ukawa unajuta baadaye kwa kitendo chako, kwa hiyo kabla hujafikia uamuzi huo, basi unahitaji kufikiri sana na kumwomba Mungu akupe hekima katika uamuzi wako. Narudia tena, unatakiwa kuwa makini sana kabla ya kufikia uamuzi wa aina hii. Unaweza kushangaa kwamba watu wanahama kanisani kwako, halafu wakienda kwenye makanisa mengine wanakuwa watenda kazi wazuri na wanaendeleza roho ya mabadiliko kwenye makanisa mapya. Kama ukiona hivyo, basi ujue kwamba shida ni wewe, na wala siyo waumini hao.
60
12. Zingatia Uwezo wa Washirika Watumishi wengi huwa tunagawa majukumu wakati mwingine kwa kupendelea bila hata kuongozwa na Roho Mtakatifu. Kama unataka mabadiliko ya haraka ndani ya kanisa hakikisha unagawa majukumu kulingana uwezo wa mtu. Bwana wetu Yesu Kristo alitupa mfano mzuri kwenye hili. Mathayo 25:14-15 Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri.” Hoja hapo niliyoiona ni kwamba “kila mtu kwa kadri ya uwezo wake.” Huyu mtu aliyesafiri, hakugawa kiholela holela tu talanta zake, bali alizingatia uwezo wao. Kwa mfano uchapa kazi wao, uwezo wao wa kuhesabu, uwezo wao wa kufanya biashara na mengine mengi. Yawezekana kuna viongozi wengine ambao hawataki mabadiliko, si kwamba hawataki, bali ni kwa sababu ya uwezo wao. Hakikisha unawapangia majukumu kulingana na uwezo wao. Kumbuka kwamba kila mtu anaweza kufanya kitu kizuri kanisani ikiwa atakuwa anacheza namba sahihi. Hebu fikiria kama goli kipa akipewa kucheza namba tano, je kutakuwa na ushindi hapo? Kwa hiyo, unapaswa kuwapanga viongozi wa mabadiliko sawasawa na uwezo wao. Ukiona mtu ana talanta fulani ya kufanya jambo kanisani, na anaonekana ana uwezo nalo, acha kuchelewa chelewa, mpe kazi hiyo afanye. Acha kufanya kila kitu wewe mwenyewe eti kwa kisingizio cha kutaka mabadiliko. Acha kusuasua, mkabidhi mtu kazi hiyo afanye, akikosea unamrekebisha, unamtia moyo, unamjenga. Mpe mtu kazi kulingana na uwezo wake. 61
13.
Mfanye Kila Mshirika Awe Shahidi
Wakristo wengi wanapokuja kanisa, husikiliza neno la Mungu kwa makini sana. Wengine huja na daftari na kalamu kwa ajili ya kuandika ujumbe unaotolewa. Wakimaliza kuhubiriwa ujumbe, basi wanaondoka. Watakutana tena siku ya maombi ya katikati ya wiki. Nao kwa uchache. Wakija wanaomba dakika kumi, wanaondoka. Wanakutana Jumapili tena. Wanasikiliza mahubiri vizuri na ibada ikiisha, kama kawaida wanaondoka. Hawafanyi kitu chochote kutokana na ujumbe ambao umehubiriwa. Hiki sicho ambacho Biblia inasema kuhusu uanachama wa kanisa. Kuwa mwanachama wa kanisa linaloonekana siyo kwenda kusikiliza neno la Mungu na kuondoka; bali ni kushiriki katika shughuli za kanisa. Na kazi kubwa ya kanisa ni kuwaleta watu wengine kwa Yesu. Nje ya kanisa linaloonekana kwa macho, kuna watu wengi ambao wanapotea. Watu wanaopotea wanahitaji mtu mmoja aliyeokoka ili aweze kuwapelekea Habari Njema ya Ufalme wa Mungu. Kwa kweli, Neno linasema kwamba, “wataaminije wasiposikia?” kwa hiyo ni kazi ya kanisa kuwaleta watu wengine kwa Yesu Kristo. Je kanisa zima linaweza kushiriki katika kuwaleta watu wengine kwa Yesu? Jibu ni ndiyo. Kuna watu ambao hudai kwamba yale maneno ya Mathayo 28:19-20 yalilenga hasa mitume 12, na kwa sababu hiyo wao hawahitaji kuhubiri Injili. Husisitiza kwamba kazi ya kuhubiri Injili ilikomea kipindi cha mitume 12 tu, na sasa hakuna haja hiyo kwa sababu Kristo anatawala mioyoni mwetu. Kwa bahati mbaya sana, fundisho hili halina mashiko Kibiblia. Ni kweli yamkini Yesu alikuwa anawaambia wanafunzi 12, lakini 62
ukisoma kitabu cha Matendo ya Mitume tunaona kwamba waliopokea Roho Mtakatifu hawakuwa wale 12 tu, bali wote. Na ahadi ya Yesu alisema kwamba, “Nanyi mtapokea nguvu akisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu.” Kwa kuwa waliokombolewa wamepewa Roho Mtakatifu, basi ni lazima wawe mashahidi wa Yesu Kristo. Mchungaji, unapaswa kumfanya kila mtu awe shahidi. Hii ndiyo kazi ambayo Yesu alituachia. Alikusudia kila mtu anayeokoka aingie shambani moja kwa moja kama shahidi. Mkristo ni shahidi wa mambo makubwa mawili; shahidi wa Ufufuo wa Yesu Kristo, na Shahidi wa maisha yaliyobadilishwa na Yesu Kristo. Kuna mtumishi mmoja aliwahi kuniambia kwamba “kanisa haliwezi kwenda zaidi ya kiongozi anavyofikiri.” Kwa kweli baada ya kupitia masomo ya kimisiolojia nimegundua kwamba ni kweli kabisa kwamba waumini hawawezi kumzidi kiongozi katika fikra zao. Hata kama waumini wa kanisa lako ni wasomi wote wa shahada ya uzamivu, bado hawawezi kufikiri zaidi ya kiongozi pale linapokuja suala la huduma na kuwaleta watu kwa Yesu Kristo. Kwa hiyo, wazo la kiongozi kuhusu kanisa ni wazo la muhimu sana. Wakati mwingine mimi huwa ninawaambia watumishi kwamba hata Mungu hawezi kufanya kitu ambacho wewe hukifikirii katika huduma yako. Najua udhaifu wa hoja hii, lakini naomba katika hili ikusaidie ili uweze kutoka hatua moja kwenda nyingine. Inawezekana wewe ukawa mbiu ya mabadiliko kanisani kwako na yamkini ukashindwa kuyaona, lakini ni bora kuwa mbiu kuliko kunyamaza. Kwa hiyo Kiongozi au mtumishi wa kanisa lazima abadilike katika fikra zake. Nitakupa dondoo chache namna ya kubadilisha washirika wako kuwa mashahidi wa Injili ya Kristo. 63
Waza Kanisa la Kimisheni Kanisa la kimisheni ni kanisa la aina gani? Mtu mmoja aliwahi kueleza kwamba Kanisa la kimisheni ni jamii ya watu wa Mungu inayojielezea yenyewe kama wakala wa Utume Mkuu wa Mungu ulimwenguni. Hili wazo linapaswa liwe wazo la kiongozi wa kanisa husika. Kiongozi hapaswi kuwa na wazo la kujaza kanisa lake tu, bali anatakiwa awaze kanisa lake kuwa kanisa la kimisheni kwa ajili ya kuufikia ulimwengu wote. Kama kiongozi hawezi kuwaza kubadilisha kanisa lake la kiasili kuwa kanisa la kimisheni, kamwe kamwe hawezi kulibadilisha likawa kanisa lenye kufikiria kufanya uinjilisti. Kanisa la kimisheni ndilo kanisa ambalo linaweza kufanya uinjilisti kwa ajili ya kuwafikia watu wengine. Kiongozi yeyote yule lazima aelekeze mawazo, nguvu, maombi na kitu kingine chochote kile kuhakikisha kwamba kanisa linakuwa linatimiza utume mkuu. Jambo linaanzia kwa kiongozi “kuwaza kimisheni,” na baada ya hapo, DNA ya kiongozi huhamia kwa washirika wote. Wanamisiolojia wengi wanaamini kwamba ili kanisa lionekane ni kanisa la kimisheni lazima liwe na sifa zifuatazo; kwanza Kanisa linalotuma wamishonari, pili, Kanisa ambalo lina kamati maalum kwa umisheni, tatu, Kanisa ambalo lina mkakati wa wazi wa umisheni, na nne Kanisa linalohusika katika huduma za mitaa na huduma za kimataifa. Nakubaliana na sifa zote hizo, lakini ningependa kusema kwamba hizo ni za kizamani sana; kwa sasa tunasisitiza watu kuwafikia watu wao. Pengine niseme kwamba
64
“kanisa la kimisheni ni kanisa ambalo linawekeza kwa ajili ya kuwafikia walio nje ya kanisa.” Kama wewe huwazi kimisheni, washirika wako hawatawaza kimisheni. Kama wewe huwekezi kwenye ufalme wa Mungu, washirika wako nao watafurahia uwepo wako wa muda; nasema uwepo wako wa muda kwa sababu hutadumu sana katika huduma hiyo.
Anza na Walio Karibu Kila muumini kanisani ana jirani yake, ana ndugu yake, ana jamaa yake, ana rafiki yake, ana mtu anayewasiliana naye wa karibu. Wafundishe watu watu kuwa na tabia ya kuwakaribisha hao ndugu zao kanisani. Kama ukiweka mkazo inawezekana kabisa kila mtu akaleta mtu mmoja kanisani ndani ya mwaka mmoja. Kuna mtu mmoja aliwahi “chuma matunda yaliyo karibu, ikiwa unaona matunda hayo yameiva.” Kwa maana ya kwamba, haina haja kupanda juu ya mti, ili kuchuma matunda yale yale ambayo pia yapo chini. Hao ndugu zako, jirani zako, rafiki zako, jamaa zako ni matunda yaliyo karibu nawe. Sasa ili uwafanye washirika wako wawe tayari kushiriki katika kazi ya Uinjilisti, unahitaji kufuata ushauri ufuatao.
Namna ya Kuwahusisha kwenye Ushuhudiaji a) Waambie waandike orodha ya watu walio karibu nao; kila mtu aandike jirani zake, ndugu zake, ana jamaa zake, ana 65
rafiki zake. Katika orodha ya kwanza waambie kila mtu angalau aandike watu watu 10 b) Waambie wafanye maombi kwa ajili ya majina hayo. Wape siku moja ya kufanya maombi kwa ajili ya watu hao. Kama ikiwezekana hakikisha na wewe unapata nakala moja ya majina yao. Kwa hiyo tuseme kwamba ukiwa na watu 10 na wakiwa na kila mmoja na watu 10 maana yake jumla utakuwa na watu 100. Kwa hiyo wewe kama kiongozi utakuwa unaomba kwa ajili ya watu mia moja kwa ujumla, lakini jukumu la kuomba kila mmoja kwa ajili ya majina hayo ni la kila mmoja. Waambie wachambue yafuatayo: i.
Nani ambaye hajaokoka katika orodha hiyo; huyu anahitaji kuombewa Habari ya wokovu wake. Omba kwa ajili ya wokovu wake
ii.
Nani ambaye ameokoka tayari-huyu unaweza kumwombea aimarishwe katika wokovu, na kumkaribisha kanisani.
Kwa kufanya hivi, kila mshirika atakuwa amepata kazi ya kufanya. Hakuna namna ambavyo anaweza kukwepa jukumu hili muhimu. c) Baada ya wiki moja ya maombi. Waambie wazungumze na hao watu waliowaorodhesha kwa Habari ya Injili. Wafundishe njia fupi ya kushuhudia injili. Kwa kawaida mimi napendekeza njia ifuatayo kama njia nyepesi ambayo mtu yeyote ambaye ameokoka anaweza kufanya:
66
d) Weka muda maalumu wa kutathmini matokeo yake. Usihangaike wewe mwenyewe, waambie wao wenyewe wakuletee tathmini. i.
Kila mtu aandike jina la mtu ambaye amemleta kanisani kupitia program hii. ii. Yule aliyeletwa kanisani apewe jukumu moja kwa moja e) Waambie kila mmoja aandike jina la mtu ambaye hakuwepo Jumapili iliyopita/au Jumapili hii. Zoezi hili litasaidia kukumbukana wao kwa wao. Kama mtu akishindwa kuandika jina la muumini mwingine, basi ujue pengine wako mbalimbali sana. Kupitia program hii watafahamiana vizuri.
Hatua za Ushuhudiaji Hatua 1: Anza na ushuhuda wako. Mara nyingi tumefundishwa kwamba anza na Injili tu. Ukianza na Injili unakata mawasiliano. Anza na ushuhuda wako. Kila mtu aliyeokoka ana ushuhuda wa namna alivyoishi kabla ya kuokoka na baada ya kuokoka. Kwa mfano “kabla ya kuokoka nilikuwa na hofu juu ya kesho yangu.” Epuka kuuliza maswali ambayo mtu anaweza kushindwa kujibu, kwa mfano, “mpendwa unamjua Yesu.” Kuna mwingine hajawahi kusikia Habari za Yesu hata mara moja.
67
Hatua ya 2: baada ya ushuhuda wako, sema moja kwa moja kuhusu Yesu Kristo ambaye amekubadilisha maisha yako. Huhitaji kufundisha, wewe sema Yesu ni Bwana mwenye kubadilisha historia ya mtu. Hatua 3: muulize kama yuko tayari umwombee na ampokee Yesu. Jaribu kuepuka majadiliano kabisa. Katika kuhakikisha kwamba kanisa zima linahusika katika kazi ya uinjilisti na kuleta mabadiliko makubwa ya uvunaji wa roho, hakikisha unasisitiza watu: a) Kuishi maisha yaliyojaa ushuhudu mzuri. Kama ushuhuda wao ukiwa mbaya hawawezi kuwashuhudia wengine kwa kanuni ambazo nimezieleza hapo juu. Kwa sababu watu moja kwa moja watajikwa kwa matendo yao. b) Hakikisha unakaza maombi. Maombi hufungua anga na mioyo ya watu kuwa laini kupokea ujumbe wa Mungu. 68
c) Ishi maisha uinjilisti, ishi maisha ya umisheni, waza kimisheni kila wakati. Ishi maisha ya Ushuhuda. Mungu akubariki.
14. Imarisha Kikundi cha Huduma kwa Wateja Unaweza kushitushwa na kichwa cha hoja hii, lakini ndio ukweli wenyewe, kwamba baada ya kuhakikisha kwamba washirika wote wanashiriki kazi ya kuwaleta wengine kwa Yesu Kristo, yaani wote wamekwisha kuwa mashahidi, kazi inayopaswa kufanyika kwa nguvu zote ni kulea hao washirika wapya ambao kila wiki watakuwa wanakuja. Nina hakika umewahi kusikia watu wakisema, “kazi siyo kushika mimba, kazi ni kulea.” Vivyo hivyo, hata kanisani kazi siyo kuwaleta watu, kazi ni kuwalea. Bwana wetu Yesu Kristo ametutuma kuzaa matunda yanayobaki, siyo yanayoondoka. Anasema kwamba. “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa;” (Yn 15:16). Tunapaswa kuwa na mikakati ya kuhakikisha kwamba matunda yanakaa. Nimetumia dhana ya kidunia “huduma kwa wateja” ingawa “waumini wapya” siyo wateja, bali ni watu wanaoungana nasi katika kumtangaza Yesu Kristo. Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba ndani ya kanisa lazima kipatikane kikundi maalumu kinachojali washirika wapya wanaokuja kila Jumapili. Ni vigumu sana kuwafanya watu wote wawe na huduma moja, ya kuhudumiana, ndiyo, ni maagizo ya Kibiblia, lakini kama kanisa lazima kuwepo na kikundi ambacho kinafundishwa kwa ustadi mkubwa namna ya kujali. 69
Mtu anapokuja kanisani, anahitaji kujisikia kwamba amekuja kwenye mikono salama; ukiachilia uhakika wa wokovu, pia anapaswa kuhakikishiwa ushirikiano, na ushirika na watu wengine. Kwa hivyo, mshirika mpya ni kama mteja katika biashara. Ni dhana ovu kutumia, lakini wacha niitumie kwa nia ya kukusaidia. Kikundi hiki cha kujali wageni na waumini wapya kanisani kinapaswa kuandaliwa kwa kuzingatia uwezo wao katika huduma. Ninaamini watu wa namna hii hawakosekani kanisani. Tahadhari wakati wa kujali 1. Msijaribu kumsaidia kimwili, kwa mfano kumpa pesa, mshirika mpya. Mkimpa tayari mmeshamjengea msingi mbovu. Ni vigumu sana kuelewa, lakini naomba uelewe hivyo, kwamba mshirika mpya asijaribu kusaidiwa kwa mahitaji yake ya kimwili. Mkimsaidia kimwili, tayari mmeshamharibu. Huyo atakuwa mshirika ombaomba. Ikiwa kweli atakuwa na mahitaji ya kimwili, basi yatolewe kwa umakini mkubwa sana, baada ya kuzingatia muktadha wa changamoto yake. Kuna watu wengi wametapeli makanisa kwa kisingizio cha kuokoka na kuja kanisani siku mbili tatu na kukopa pesa, au kuchangiwa kwa madai ya kukosa makazi, na mara walipopata kile wanachotaka, basi hawaonekani tena. Ni kweli kanisa linaweza kumsaidia mtu yeyote, hata mpagani kabisa, lakini asitumie mgongo wa wokovu, bali aombe msaada tu. Nina hakika makanisa yetu yanafanya hivyo mara nyingi. 2. Siku hizi, msifanye haraka sana kwenda nyumbani kwake, isipokuwa kama amewakaribisha, au vinginevyo tumieni hekima. Watu wengi siku hizi hawataki watu waende kwenye nyumba zao kwa sababu unakuta labda amepanga chumba kimoja, yeye na watoto wake, na kila kitu kiko hapohapo 70
chumbani, sasa mwingine anaona aibu. Mnaweza kuwa na nia ya kujali na kutaka kushirikiana naye, lakini tumieni hekima, au mpaka atakapozoea, basi mnaweza kwenda kwake na kushirikiana naye. Tunapaswa kukumbuka kwamba siku hizi huduma ya kutembelea imebadilika. Simu zetu zinapaswa kutumika vizuri katika kuwatembelea watu. Chukua namba ya simu ya mtu, weka ratiba ya kuwapigia wote ama kutuma ujumbe mfupi wa maneno kwa kuwatia moyo, kuwahakikishia kwamba uko pamoja nao, na unawaombea.
71
Historia ya Mwandishi Daniel John Seni, ni mchungaji. Alimuoa Esther Mligo mwaka 2011. Alizaliwa miaka 40 iliyopita katika wilayani Meatu, Mkoani Simiyu Alisoma katika shule ya Msingi Tindabuligi kati ya Mwaka 1990-1997. Baada ya kumaliza elimu ya msingi, hakupata alama za kutosha kuruhusu aende sekondari, na badala yake aliendelea kujishughulia na shughuli za kilimo nyumbani kwao Tindabuligi kuanzia mwaka 1997-2002. Mwaka 2002 alipata wito wa kumtumikia Mungu na alitumika chini ya kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) kama mwinjilisti, kijijini kwao. Na mwaka 2003 alienda kusoma katika chuo cha Biblia Kolandoto (Kolandoto Bible School) kilicho chini ya Kanisa AICT. Akiwa chuoni, alikutana na Mmissionari kutoka Korea Mwl Boyeon Lee, ambaye aliamua kufanya kazi pamoja naye. Na kuanzia hapo, alianza kujiendeleza kwa kusoma elimu ya watu wazima na kufanya mtihani wa QT mwaka 2005. Desemba 2005, alihamia Dar es salaam, na baadaye mwaka 2006, alijiunga na chuo cha Calvin Theological College, (CTC) kilicho chini ya Korea Church Mission Tanzania (KCM). Akiwa anaendelea na masomo ya Theologia, huku akijiendeleza na masomo ya watu wazima, mwaka 2007 alifanya mtihani wa Kidato cha Nne, na mwaka 2010 alifanya mtihani wa kidato cha Sita. Mwaka 2013 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es salam na kusoma kozi ya BA.Kiswahili, na kuhitimu mwaka 2015. Mch. Daniel J. Seni alisimikwa kuwa mchungaji rasmi katika kanisa la Presbyterian Church in Tanzania Julai 2014. Mwaka 2016 alijiunga na chuo kikuu cha Chongshin Theological Seminari nchini Korea Kusini kwa ajili ya shahada ya 72
Uzamili, na kuhitimu mwaka 2019 alihitimu. Mwaka 2020 alijiunga na Chuo cha Calvin Graduate School of Theology nchini Korea Kusini kwa ajili ya kusoma kozi ya Shahada ya Uzamivu, ambapo mpaka sasa bado ni mwanafunzi. Mch. Daniel J. Seni kwa sasa ni mchungaji kiongozi wa kanisa la Shekinah Presbyterian Church in Tanzania. Mch. D.J. Seni ni mwandishi wa vitabu vifuatavyo 1. Uwezekano wa Mkristo Kupagawa pepo 2. Upandaji wa Makanisa 3. Tamthiliya ya Mzee Maduhu 4. An anaysis of Westimister Confession of Faith: Pneumatological Approach (amazon) 5. The Inevitability of Women’s Ordination (amazon) 6. Dhana ya Mafanikio 7. Namna unabii wa Media unavyokinzana na Nabii za Kibiblia (Amazon) 8. Njoni Tuabudu: Taratibu za Ibada Hivi karibuni amejikita katika uandishi wa vitabu vya mafundisho ya msingi ya kanisa (Church Doctrines) na miswada iliyo tayari ni:1. Ekklesiolojia 2. Anthropolojia 3. Soteriolojia Mch. Daniel J. Seni ametafsiri katika Kiswahili vitabu vifuatavyo:1. The Westminster Shorter Catechism 2. The Westminster Larger Catechism 3. The Westminster Confession of Faith
73
74